Eric Omondi, Carol Katrue wasifiwa huku Miracle Baby akiruhusiwa kutoka hospitali baada ya miezi 2

Bili ya takriban Ksh 1.4 millioni ililipwa Ijumaa baada ya Eric Omondi kuhamasisha Timu yake Sisi kwa Sisi kuchanga pesa..

Muhtasari

•Miracle Baby hatimaye aliruhusiwa kuondoka hospitalini siku ya Ijumaa jioni baada ya bili ya takriban Ksh1.4milioni iliyokuwa imesalia kulipwa.

•Carol Katrue pia amepokea sifa nyingi kwa kusimama na mpenzi huyo wake na kumtunza katika miezi miwili iliyopita.

aliruhusiwa kutoka hospitali Ijumaa
Miracle Baby aliruhusiwa kutoka hospitali Ijumaa
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji mashuhuri Peter Mwangi almaarufu Miracle Baby hatimaye aliruhusiwa kuondoka hospitalini siku ya Ijumaa jioni baada ya bili ya takriban Ksh1.4milioni iliyokuwa imesalia kulipwa.

Bili kubwa ambayo ilikuwa imefanya msanii huyo wa gengetone kuzuiliwa hospitalini hatimaye ililipwa Ijumaa baada ya mchekeshaji Eric Omondi kuingilia kati na kuhamasisha Timu yake Sisi kwa Sisi kuchanga pesa..

Wakati akitangaza habari njema za kuachiliwa kwa mwimbaji huyo kutoka hospitalini, Eric Omondi aliwapongeza mashabiki wote waliochangia na kuwaombea baraka.

“MUNGU ANA FURAHA!!! MUNGU AWABARIKI KILA ALIYETUMA CHOCHOTE...Mungu anakuona. Ndugu yetu ametoka Hospitali baada ya siku 60 kwa sababu yako.

TIMU YA SISI KWA SISI Yaani mkisemanga ni leo lazima ikue leo🙏🙏🙏,” Eric Omondi alisema.

Mchekeshaji huyo wa zamani wa kipindi cha Churchill pia alitumia fursa hiyo kumsifu mpenzi wa Miracle Baby Carol Katrue kwa kusimama naye katika kipindi chote cha ugonjwa wake.

 "AHSANTE Kubwa sana kwa mke wa Miracle baby Carol Katrue, yaani huyu msichana aliamua lazima bwana yake arudi nyumbani, alikaa naye mchana na usiku," alisema.

Akaongeza, “MUNGU AWABARIKI NYOTE. @petermiraclebaby hajafanya kazi kwa muda wa miezi 4 iliyopita bado unaweza kutuma kitu kwa ajili yake na Familia kupitia mke wake Carol kwa nambari 0794790255 ((JINA: CAROL MBUTHIA).

Eric aliambatanisha taarifa yake na video iliyomuonyesha Miracle Baby akiruhusiwa kutoka hospitalini, tukio ambalo lilijawa na nyimbo na shangwe za watu wakisherehekea maendeleo hayo mapya.

Katika video hiyo, msanii huyo wa gengetone alionekana akitabasamu kwa furaha huku akitangamana na watu hospitalini na kukata keki kusherehekea.

Mwimbaji huyo ambaye alikuwa amevalia kaptura na shati la mgonjwa pia alionekana akifanya sala wakati akitoka hospitalini na kuingia kwenye gari lililompeleka nyumbani.

Kufuatia msanii huyo wa gengetone kuachiliwa kutoka hospitali, mchekeshaji Eric Omondi amesifiwa sana kwa kutumia ushawishi wake kuhamasisha watu kuchanga pesa.

Carol Katrue pia amepokea sifa nyingi kwa kusimama na mpenzi huyo wake na kumtunza katika miezi miwili iliyopita ambayo amekuwa mgonjwa.

Miracle Baby amekuwa hospitalini kwa siku 60 zilizopita ambapo amefanyiwa upasuaji mara tatu ili kurekebisha matatizo ya utumbo aliyokuwa nayo. 

Bili ya zaidi ya Ksh 1.5 milioni imekusanywa katika kipindi chote cha kulazwa hospitalini.