
SEHEMU ya wachungaji katika kaunti ya Meru wamesema hawawezi kata michango ya pesa kutoka kwa wanasiasa huku rais Ruto akitarajiwa kutembelea kaunti hiyo katika ziara yake ya wiki moja eneo la Mlima Kenya.
Wakizungumza na waandishi wa habari
katika kaunti hiyo, wachungaji hao walisema kuwa hawawezi kataa pesa kwani
hakuna pesa chafu wala ya dhambi.
“Kuna pesa tunaona
zikipatiwa makanisa, unapata maaskofu wa kanisa kubwa kubwa wanasema pesa
irudishwe. Sasa tunashangaa kama mimi hata kama naheshimu mafuta naheshimu kina
baba wa kanisa, ningependa kuuliza kwa unyenyekevu, kuna ile njia inaweza tumika
zinaweza saidia watu kwa sababu pesa si eti ni ya dhambi, hakuna pesa ya
dhambi,” Alisema pasta Jediel Kirema.
Mchungaji huyo alisisitiza kwamba
wachungaji wanahitaji pesa hizo kujikimu kimaisha ili kuweza kueneza injili kwa
mwenendo unaofaa.
“Yale makanisa ambayo yanarudisha pesa
mle ndani kuna makahaba, kwa kuwa hujui nia ya mtu, kuna wezi… na wote wanatoa
pesa. Kwa hivyo pesa ni ya benki kuu ya Kenya, pesa haina shida, iletwe kwa
njia za utaratibu.”
“Ziletwe ili zisaidie wachungaji
wengine waache kutumia njia za ujanja kutafuta pesa, wakipata pesa za kujimudu
kibiashara hata kazi ya Mungu itafanyika kwa njia halali, kwa hivyo hakuna pesa
mbaya, rais pesa si mbaya, imetengenezwa na ni ya Mungu,” Kirema aliongeza.
Askofu James Gichuru pia aliradidi maneno hayo akisema kwamba rais Ruto amekaribishwa kutoa sadaka katika makanisa yao na kuahidi kwamba wao hawatarudisha sadaka.
“Tunajua na tumesikia kwamba mheshimiwa
rais Ruto anakuja Meru. Sisi wachungaji tunamkaribisha Meru na tunamuomba pia
akija asapoti sacco za wachungaji. Pesa kama zile zinapeanwa tukipewa sisi kama
sacco zitasaidia wanachama wetu na tutaweza kujimudu, hatutakuwa watu wa kuomba
omba, tutakuwa watu wa kujisimamia na kufanya mambo,” askofu huyo alisema.
Askofu huyo alibainisha kwamba wao
hawako katika siasa bali wanaunga mkono uongozi wa serikali iliyopo kutoka kwa
ngazi za kaunti hadi kitaifa.