
MSANII na mkurugenzi mkuu wa wakfu wa Simple Boy, Stevo Simple Boy amewaonya wanaume wanaotafuta wanawake wa kuoa dhidi ya kukimbilia wale wanaojitambulisha kama wameokoka.
Akizungumza na Obinna TV Updates, Stevo Simple Boy alisema
kwamba siku hizi ni rahisi sana kupata mwanamke ambaye ni mtiifu, anamuogopa
Mungu lakini bado akawa si mke mwema.
Kulingana naye, mrembo anaweza akawa mke mwema bila hata ya
kuwa mtiifu au mwenye ameokoka.
“Wacha niwaambie kitu
kimoja, unaweza pata msichana ameokoka, ni mtiifu, lakini bado asiwe mke mwema,” Simple Boy alisema.
Msanii huyo mwenye misemo na Kauli za kutatanisha alionekana
kuegemea dhana kwamba kuna uwezekano wa kupata mwanamke anayetumia dawa za
kulevya lakini akaibukia kuwa mke mwema.
Msanii huyo hata hivyo alisema ukifika wakati wake wa
kutafuta mke, ataangalia vigezo vya utiifu, unyenyekevu na mchapa kazi.
“Mimi kwa sasa sitafuti
mtu lakini ukifika huo wakati, kwanza lazima awe mchapa kazi, mchamungu, na
mnyenyekevu,” alisema.
Akijibu kwa nini amekawia kupata mchumba, msanii huyo alisema
kwamba amekuwa na ugumu kumpata ambaye atampenda yeye kama Stephen wa maisha
halisi na si Stevo wa mitandaoni.
“Mimi siwezi sema eti
naona sai wala mtondogoo, yule mwenye atakuja si eti anakuja juu ya Stevo
Simple Boy, akuje juu anapenda Steven. Unajua Stevo Simple Boy ni wa mitandaoni
na Stephen ni wa nyumbani,” alibainisha huku akikataa kabisa
kuzungumzia uvumi wa kesi yake na aliyekuwa mkewe kuhusu suala la mtoto.