Akothee akasirika baada ya aliyemuuzia dawa ya kusaidia uzazi kuropoka kwenye ukurasa wake

Alisema nusura aache kwenda kununua vitu madukani kwa sababu ya watu kumpiga picha ovyoovyo wakiwemo wale wanaomuuzia.

Muhtasari

•Akothee amewaonya mashabiki wake dhidi ya kumkaribia wakati akiwa hadharani huku akiwa amefunika uso wake kwa barakoa.

•Alisema kwamba huwa anaona watu wageni wanaomjia kama washukiwa haswa akiwa peke yake bila walinzi.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amewaonya mashabiki wake dhidi ya kumkaribia wakati akiwa hadharani huku akiwa amefunika uso wake kwa barakoa.

Katika taarifa yake siku ya Jumapili, mama huyo wa watoto watano alidokeza kwamba hapendi watu wakimsalimia au kumpiga picha akiwa katika harakati zake za kibinafsi.

"Inanifanya nihisi kama mimi huwa chini ya uchunguzi kila wakati. Hii inanikasirisha, watu hao watakataa wakati ukikabiliana nao na kuuliza ikiwa wanakupiga picha. Kwa hakika, wako tayari kila wakati kupigana," alisema.

Akothee alifichua kuwa hapo awali aliwahi kukabiliana vikali na mashabiki wake katika maeneo ya umma kwa mfano viwanja vya ndege, mikahawa na maduka makubwa. Alifichua kuwa nusura aache kwenda kununua vitu madukani kwa sababu ya watu kumpiga picha ovyoovyo wakiwemo wale wanaomuuzia bidhaa.

“Tukio baya zaidi, niliingia kwenye duka la dawa kununua dawa yangu ya uzazi (pregnacare) akaja mmoja wa mfamasia kutoa maoni kwenye ukurasa wangu, "nilikuhudumia jana kwa duka letu la dawa, njoo tena" .Nilikuwa na MASK mbona nyie watu mfanya hivi?" Alilalamika.

Mwanamuziki huyo aliibua malalamishi hayo baada ya mwanadada mmoja aliyedai kukaa naye kwenye ndege kutoka Mombasa kumpiga picha bila idhini kisha baadaye kumtumia ujumbe pamoja na picha hiyo.

"Millicent, mbona hukuomba picha. Hii umeiba kwa nini? Upeleke wapi mgongo yangu? Nyinyi ndio mnafanya nakufa ndani ya barakoa," Akothee alimlalamikia mwanadada huyo na kuambatanisha na ujumbe aliomtumia.

Aliongeza, "Kuna sababu ya mimi kujifunika wakati wa kusafiri au katika mazingira magumu zaidi. Inaitwa camouflage, unaponiona hivi tafadhali naomba unipuuze. Siko kwenye mood, hata wa kusalimiana. "

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alifichua kuwa matukio yake mabaya ya zamani na mashabiki wake yalimfanya kuwa mwangalifu zaidi kuhusu mwonekano wake katika maeneo ya umma na jinsi anavyojihusisha na watu anaokutana nao.

Alisema kwamba huwa anaona watu wageni wanaomjia kama washukiwa haswa akiwa peke yake bila walinzi.

"Ukiona chapisho langu kuhusu shoo au kuonekana hadharani, piga picha nyingi unavyotaka, ni date yetu. Maisha ya umma ni ya kuudhi, yanachosha," alisema.