"Aliubeba kwa neema na upendo" Juliani afufua kumbukumbu za ujauzito wa mkewe Lilian Ng’ang’a

Juliani na Lilian walimkaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja duniani, Utheri, mnamo mwezi Julai mwaka jana.

Muhtasari

•Katika ujumbe wake kwa mpenzi huyo wa zamani wa waziri Alfred Mutua,  Juliani alimshukuru kwa kubeba ujauzito wa mtoto wao, Utheri.

•Aliendelea kumtakia mama huyo wa mtoto mmoja kheri ya siku ya akina mama na kumtambua kama mke wake.

Lilian Nganga na mumewe Juliani
Image: INSTAGRAM// JULIANI

Siku ya Jumapili, Mei 14, dunia nzima iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Akina Mama ambapo mamilioni ya walimwengu walitumia siku hiyo kusherehekea akina mama maalum katika maisha yao kwa njia tofauti.

Rapa Julius Owino almaarufu Juliani alijumuika na walimwengu wengine katika sherehe hizo kwa kumuonesha upendo mke wake Lilian Ng’ang’a.

Katika ujumbe wake kwa mpenzi huyo wa zamani wa waziri Alfred Mutua,  Juliani alimshukuru kwa kubeba ujauzito wa mtoto wao, Utheri.

"Min Ler hapa akiwa mja mzito lakini mapua haukufura. Aliibeba kwa neema na kwa upendo mang'eng," Juliani alisema kwenye Instagram na kuambatanisha na picha ya kumbukumbu ya mke huyo wake wakati akiwa mjamzito.

Aliendelea kumtakia mama huyo wa mtoto mmoja kheri ya siku ya akina mama na kumtambua kama mke wake.

akiwa mjamzito.
Lilian Ng'ang'a akiwa mjamzito.
Image: INSTAGRAM// JULIANI

Mwimbaji huyo na mkewe Lilian Nganga walimkaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja duniani, Utheri, mnamo mwezi Julai mwaka jana, takriban mwaka mmoja tu baada ya kuyaweka wazi mahusiano yao.

Akizungumzia jinsi ulezi wa Utheri umekuwa mnamo mwezi Machi, mke huyo wa zamani wa waziri wa Masuala ya Kigeni Alfred Mutua alibainisha kuwa imefufua baadhi ya mambo ya kitoto aliyofanya miaka ya nyuma.

"Kulea mtoto huyu kumeamsha utoto ulio ndani yangu ambao ulikuwa umesahaulika kwa muda mrefu," Bi Nganga alisema.

Mama huyo wa mvulana mmoja aliweka wazi kuwa anafurahia sana hatua ya kumlea mwanawe na mambo ambayo imemlazimu kufanya.

"Ninaipenda kwa ajili yangu.. kwa ajili yake.. kwa ajili yetu," alisema.

Juliani alifichua kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza na mkewe Lilian Nganga akiwa kwenye mahojiano mapema mwezi Agosti.

Akizungumza na Presenter Ali, mwimbaji huyo wa nyimbo za kufoka alitangaza habari kwamba walipokea zawadi ya mtoto wa kiume siku zilizokuwa zimepita na kuweka wazi jinsi alivyofurahi kuwa baba tena.

 "Nina watoto wawili. Msichana na mvulana. Nilimkaribisha mtoto wa kiume hivi majuzi na Lilian Ng'ang'a," alisema.

Juliani na Lilian walifunga ndoa katika Paradise Lost mnamo Februari 2, 2022, mbele ya familia na marafiki wa karibu.

Orodha ya wageni ilikuwa chini ya watu 50. Ilikuwa wakati huo ambapo Wakenya waligundua Lilian alikuwa anatarajia mtoto.