'Msiogope kutumia pesa zenu kuonekana vizuri,' Murugi Munyi ashauri

Muhtasari

• Mwanablogu Murugi Munyi amewashauri watu wasiogope kutumia pesa zao kutafuta muonekano mzuri wa mwili.

• Akizungumza na mtangazaji Massawe Japanni, Munyi alisema kwamba yeye alipoona mwili wake unanenepa visivyo, alitumia kiasi cha laki sita (600,000) za Kenya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mafuta kwa mwili

Murugi Munyi
Image: Mercy Mumo

Mkuza maudhui Murugi Munyi ambaye alibadilisha jina lake la mitandoni kutoka lile la awali la Yummy Mummy amewashauri watu wasiogope kutumia pesa zao ili kutafuta muonekano mzuri wa miili yao.

Akizungumza na mtangazaji Massawe Japanni, Munyi alisema kwamba yeye alipoona mwili wake unanenepa visivyo, alitumia kiasi cha laki sita (600,000) za Kenya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mafuta kwa mwili wake na kubadilisha muonekano wake. Upasuaji huo kwa lugha ya kitaalamu unaitwa liposuction.

Munyi alisema kwamba hakushrutishwa na yeyote kutumia kiasi hicho kikubwa cha pesa ili kubadilisha umbo la mwili wake kwani alikuwa na nafasi ya kuchagua kati ya liposuction na kufanya mazoezi ya kunyanyua vyuma ila akaamua tu kuendea upasuaji kwa sababu alikuwa na pesa.

“Niliamua kuendea upasuaji wa lipo kwa sababu nilikuwa na pesa na kwa kuwa ilikuwa ni kujibamba kwa siku yangu ya kuzaliwa. Kama binadamu unapata tunatia bidi sana katika kutafuta pesa ili kumudu vitu tunavyovihitaji, haikuwa pesa nyingi bali ni chini ya laki sita tu. Ni pesac ambayo nimeifanyia kazi kwa jitihadqa kubwa na ilitoka mfukoni mwangu. Ninahisi mwenye ujasiri mara mia moja Zaidi ya awali,” alisema Munyi.

Mapema kabla ya mahojiano hayo ya kipekee kwenye redio, Munyi alikuwa ameandika kwenye Instagram yake kwamba amepunguza lita 8.7 za ufuta kutoka mwilini kupitia kwa upasuaji wa lipo.