Wasioamini Mungu Kenya wanataka marufuku ya maombi shuleni

Muhtasari

• Wasioamini uwepo wa Mungu nchini Kenya wanataka waziri Magoha kufutilia mbali taratibu za kidini katika shule za serikali humu nchini.

• Wanasema kulazimishiwa maombi ni hatia katika katiba ya Kenya ya mwaka 2010 kifungu cha 32.

Harrison Mumia
Image: Instagram

Muungano wa wasioamini uwepo wa Mungu nchini Kenya, (Atheists)  unaitaka wizara ya elimu na serikali kwa jumla kupiga marufuku maombi shuleni, haswa nyakati hizi ambazo shule zinajiandaa kwa mitihani ya kitaifa KCSE na KCPE.

Katika barua ambayo iliandikiwa wizara ya Elimu na kutiwa Saini na rais wa muungano huo Harrison Mumia, muungano huo umemtaka Waziri wa elimu profesa George Magoha kupiga marufuku shughuli zozote zinazoendana na kufanyia wanafunzi maombi shuleni ili kujiandaa kuukabili mtihani wa kitaifa.

Pia wamemtaka Magoha kupiga marufuku ya wanafunzi kulazimishiwa kufuata miendendo fulani inayohusiana na dini shuleni wakisema kwamba wamepokea malalamiko mengi kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu hulka za shule kulazimishia wanafunzi taratibu za kidini ambazo hawazitaki.

“Tumepokea malalamishi mengi kutoka shule za upili za serikali kwamba wanalazimishia wanafunzi kufuata taratibu za kile wanachokiita siku za maombi. Kisa cha hivi karibuni kikiwa ni kile cha mwanafunzi kutoka shule ya mesto ya Kinjo iliyoko kaunti ya Meru kwamba mwalimu mkuu aliandaa siku ya maombi Februari 23 shuleni humo na kusema ni lazima kila mwanafunzi ahudhurie. Hili halikubaliki,” sehemu ya barua hiyo inasoma.

Barua hiyo inaendelea kusema kwamba kulazimishia watu maombi kumeharamishwa katika katiba ya Kenya ya mwaka 2010 na kwamba sehemu za shule ni za masomo kwa wanafunzi wa dini zote na haifai kulazimishiwa kufuata kanuni fulani za dini ya shule hiyo.

Image: INSTAGRAM
Image: INSTAGRAM