Samidoh, Amerix, Andrew Kibe, Omar Lali - Waliopendekezwa kumrithi Kibor

Muhtasari

Mzee Kibor aliaga dunia mapema Alhamis na tayari mchakato wa kumtafuta mtu wa kuziba pengo lake kama mwenyekiti wa vuguvugu la kutetea maslahi ya jinsia ya kiume umechacha mitandaoni.

Marehemu Jackson Kibor
Marehemu Jackson Kibor
Image: MAKTABA

Mzee Jackson Kibor ambaye alikuwa amebandikizwa jina la majazi kama mwenyekiti wa kundi la kutetea masllahi ya mtoto wa kike alifariji mapema Alhamis wiki hii.

Kifo chake kilifungua ukurasa mwingine wa mijadala mikali mitandaoni kuhusu ni nani haswa atakayerithi mawanda yake kama mtetezi wa maslahi ya jinsia ya kiume hyumu nchini, ambaye pia atakuwa mwenyekiti wa mikutano ya wanaume inayofanyika kila mwaka siku kuu ya Valentino.

Huku wengine wakiendelea wakimuomboleza mzee Kibor na kutuma salamu za rambirambi, baadhi wameanzisha mchakato wa kuwapigia debe wanaume ambao wanahisi wako na vigezo hitajika katika kuchukua mikoba ya mzee.

Ilianza na mwanasiasa anayewania Useneta kaunti ya Nairobi, mwanamama Karen Nyamu ambaye alianzisha mjadala huo kwa kumpendekeza mchepuko wake Samidoh kama mrithi wa Kibor.

Hili halikuishia hapa kwani baadhi ya ‘wanakamati’ wa vuguvugu hilo waliorodhesha vigezo ambavyo kidogo vilionekana kutompendelea Samidoh ambapo walisema nafasi hiyo inafaa sana kwa mtu ambaye kidogo umri umepiga hatua na kusema kwamba Samidoh bado ni kijana mbichi.

Baadhi walipendekeza katibu wa muungano wa wafanyakazi nchini Francis Atwoli kuchukua nafasi hiyo huku wengine wakimtaja mshawishi maarufu kwenye mtandao wa Twitter kwa jina Amerix kama chaguo bora.

Majina mengine zaidi yaliibuka ambapo wanamitandao walimtaja aliyekuwa mtangazaji na ambaye kwa sasa ni mkuza maudhui katika mtandao wa YouTube, bwana Andrew Kibe kuwa mtetezi bora wa maslahi ya kiume.

Na kama haitoshi, wengine walimtaja ‘beach boy’ Omar Lali kuchukua nafasi ya Kibor. Lali aligonga vichwa vya habari miaka michache iliyopita kwa kushtakiwa dhidi ya kifo cha mtoto wa mfanyibiashara wa kampuni ya vileo ya Keroche.

Bila shaka, mjadala huu bado unaendelea katika mitandao ya kijamii na dalili zote zinaashiria huenda kumpata mtu wa kuliziba pengo lililoachwa na marehemu mzee Kibor ni mchongoma wa kuupanda, kwani badowanamitandao wengi wanazidi kutofautiana na kila jina linalotajwa kama mbadala wa Kibor.

Unahisi nani mweye uwezo wa kuziba pengo la Kibor kama mwenyekiti wa vuguvugu la kutetea haki za mtoto wa kiume?