Flaqo apewa msomo na babake kwa video 'isiyoridhisha'

Muhtasari

• Hiyo video uliipakia mwezi Juni 2019 na haipendezi kabisa katika ushauri wangu. Hii ingine mpya pia haikai sawa kabisa na mimi, inanichanganya, hebu nipigie simu mara moja - Babake Flaqo

Mchekeshaji Flaqo Raz
Mchekeshaji Flaqo Raz
Image: Instagram

Mchekeshaji Flaqo ama Mama Othis kama ambavyo anatambulika na wengi kutokana na ‘skits’ zake amewaacha wengi baada ya kufichua kwamba babake alimpa msomo uliohitimu baada ya kuachia video ya ngoma yake mpya kwa jina Insincere.

Akiandika kwenye Instagram yake, Flaqo alisema kwamba baada ya babake kuona video hiyo, alimtafuta mara moja na kutaka kujua mbona mchekeshaji huyo alifanya video kama hiyo ambayo ilimtatanisha.

Katika ‘screenshots’ hizo za mazungumzo na babake, Flaqo anaonekana akiwa kikaangani huku babake akimtaka aelezee mbona anaenda kinyume na wosia wake ambapo pia ilitambulika baba mzazi aliwahi mpa onyo tena wakati alitoa video ingine yenye utata mwaka 2019.

Baada ya Flaqo kushindwa kujieleza kwa njia ya kumshawishi babake ili aelewe kiini na maana ya video hiyo mpya, babake alitoa amri ya mchekeshaji huyo kumtafuta kwa kumpigia simu haraka iwezekanavyo.

“Kuna video ambayo wakati mmoja nilikuzungumzia kuihusu na naona haioneshi kile ambacho ninataka na kutarajia kutoka kwako, hiyo video uliipakia mwezi Juni 2019 na haipendezi kabisa katika ushauri wangu. Hii ingine mpya pia haikai sawa kabisa na mimi, inanichanganya, hebu nipigie simu mara moja!” Ujumbe wa babake unasema.

Mchekeshaji huyo ambaye anajaribu guu lake katika utunzi wa muziki alijitahidi kujitetea kwamba matukio katika video hiyo ambayo muigizaji Carrol Sonie anakipiga kama video vixen ndio yanasimulia uhalisia wa beti za wimbo wake lakini yote yaliambulia patupu ambapo babake alisisitiza amtafute kwa njia ya simu.

“Sitaki kusema kwamba mimi ni mtoto wa baba lakini wueeh mimi hupitia msomo sana kutoka kwa babangu kuhusiana na maudhui ninayoyafanya,” aliandika Flaqo.