Hatimaye mzee Oribo kuzikwa baada ya mwili kukaa mochari kwa miaka 6 kwa kesi ya shamba

Waziri wa usalama Dkt. Fred Matiang'i aliingilia kati katika kutatua mzozo huo wa shamba uliokawia kwa miaka 6 mwili wa Oribo ukiwa mochwari.

Muhtasari

• Inadaiwa mlalamishi aliibuka baada ya mzee Oribo kufa na kusema aliuziwa shamba hilo lote mwaka 1969.

• Baada ya matiang'i kuingilia kati, ilifahamika mzee Oribo hakuuza shamba lote na sasa atazikwa katika kipande cha shamba kilichosalia.

• Kesi hiyo ilikuwa imekawia mahakamani kwa miaka 6 huku mwili wa mzee ukiwa bado makafani ya hospitali ya rufaa ya Kisii.

Maziara
Maziara
Image: The Star

Miezi michache iliyopita,  palizuka hadithi ya kuvunja moyo kuhusu familia moja kaunti ya Kisii ambao walishindwa kumzika mpendwa wao kutokana na mzozo wa ardhi ambapo mtu mmoja alitokea na kudai mzee wa boma hiyo ambaye alikuwa amekufa alimuuzia shamba lake lote na hivyo kuzuia mwili wake kuzikwa hapo.

Katika hadithi hiyo iliyoangaziwa na vyombo vya habari vya humu nchini, mzee huyo alifariki na kulazimu mwili wake kusalia katika chumba cha kuhifadhi maiti kwa zaidi ya miaka sita huku kesi ya mzozo wa ardhi baina ya familia yake na mtu aliyedai kuuziwa shamba hilo ikijikokota kortini miaka hiyo yote.

Inasemekana mzee huyo kwa jina Oribo kutoka maeneo ya Kiamokana kaunti ya Kisii aliuza shamba lake mwaka 1969 na alipofariki miaka 6 iliyopita, mwenye shamba ambaye alinunua na kumpa Oribo na familia yake idhini ya kuendelea kukaa kwenye shamba hilo alizuka na kudai shamba lake pazizikwe mtu.

Baada ya familia hiyo kuhaingaika kwenye milango ya mahakama kwa miaka sita, hatimaye wamesalimika baada ya Waziri wa usalama Dkt. Fred Matiang’i kuingilia kati katika mzozo huo na kuleta utatuzi ambapo familia hiyo imeruhusiwa kumzika mpendwa wao baada ya kubainika kwamab mzee huyo hakuuza shamab lake lote kama ambavyo mlalamishi alikuwa anadai bali ni sehemu kidogo tu.

Siku chache zilizopita wakati Waziri Matiang’i alikuwa kweney mahojiano ya kipekee na kituo kimoja cha redio humu nchini, watu wengi walimtaka kuzungumzia suala hilo ambapo aliahidi kuingilia kati ili familia hii ipate haki, ahadi ambayo alitimiza siku chache baadae. Matiang’i pia aliahidi kuwajengea wanafamilia hii nyumba katika sehemu ya shamba ambalo lilibaki.

Katika picha ambazo zilipakiwa mitandaoni, inasemekana Waziri Matiangi hatimaye aliwajengea waanfamilia hao nyumba mbili na mzee Oribo anatarajiwa kupumzishwa leo hii baada ya kushinda katika makafani ya hospitali ya rufaa ya Kisii kwa miaka 6.

Mzozo huu ulizuka baada ya wanaharakati na watetezi wa haki za kibinadamu wakiongozwa na Samwel Okemwa ambaye analenga kuwa seneta wa kaunti hiyo, kuingilia kati na vyombo vya habari kuliangazia Sakata la familia hiyo.