"Ujauzito wangu haukupangwa" Diana Marua afichua sababu za kuficha ujauzito wake

Diana alieleza kuwa alichukua muda wake kukubali kuwa ni mjamzito

Muhtasari

•Diana Marua alifichua kuwa ujauzito huo wake wa tatu ulimpata kwa mshangao kwani hakuutarajia.

•Diana aliwataka Wakenya kuangazia mambo yao wenyewe na kuyaheshimu maisha ya kibinafsi ya watu wengine. 

Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwanavlogu Diana Marua amekiri kuwa yeye na mumewe Bahati hawakupanga ujauzito anaoubeba sasa.

Katika mahojiano na Eve Mungai, Diana alifichua kuwa ujauzito huo wake wa tatu ulimpata kwa mshangao kwani hakuutarajia.

"Sikukaa chini nikasema nataka Heaven ama Majesty. Ujauzito wa Heaven na Majesty ulikuwa umepangwa. Hii ingine ilibackfire. Ilikuwa mshangao," Diana alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alisema kuwa alichukua muda wake kukubali kuwa ni mjamzito na ndiyo maana hakukurupuka kuwatangazia mashabiki wake kuhusu habari hizo.

"Ilikuwa ni wakati wangu kukubali niseme kwa kuwa imetokea ni lazima nikubali hali hiyo na wakati nitakuwa sawa kuhusiana nalo nitatangaza  kwa umma," Alisema.

Rapa huyo anayejitabulishwa kwa jina la kisanii Diana B pia alibainisha kuwa ni uamuzi wake kutangaza ujauzito anapotaka kutangaza.

Aliwataka Wakenya kuangazia mambo yao wenyewe na kuyaheshimu maisha ya kibinafsi ya watu wengine. 

"Siko hapa kushinikizwa na umma. Ata kama nitatembea na muone umma ikiwa bado sijatangaza, ni nafasi yangu kutangaza," Alisema.

Katika mahojiano hayo, mke huyo wa Bahati pia alidokeza kuwa angependa mtoto wake  wa tatu awe msichana.

Diana na mumewe Bahati walitangaza ujauzito wao wa tatu kutia wimbo 'Nakulombotov' mnamo Julai 15.

Wawili hao walionyesha ujauzito mkubwa wa Diana kwa mara ya kwanza katika video ya wimbo huo uliopakiwa kwenye YouTube.

"Baraka nyingine..  Asante Mungu," Diana aliandika chini ya video ya wimbo huo.

Katika wimbo huo wa dakika tatu wanandoa hao walitoa ahadi kemkem na ushauri kwa mtoto wao ambaye hajazaliwa.

Wawili hao pia walimhakishia mtoto wao kuhusu upendo wao mkubwa kwake na kumtakia baraka tele maishani.

"Nakutakia baraka, nakutakia fanaka,

Nakutolea sadaka, nyota yako itawaka,

Utamkia neema isiyokuwa na mipaka.

Maisha mazuri, uishi mamiaka.

Magonjwa na mikosi na zikae mbali,

Malaika wakulinde dhidi ya ajali.

Hekima ikutawale kama serikali,

Nasi tunakusubiri kama fainali,"  Diana alisema katika kipande cha wimbo huo.

Diana pia alimfahamisha mwanawe ambaye hajazaliwa kuhusu jinsi  dunia ilivyo huku akimueleza kuwa kwa kawaida mambo sio rahisi.