Kajala amsherehekea Harmonize baada ya kumwaga mamilioni kumnunulia iPhone 14

"Hommie Wangu katisha!" Kajala alisema.

Muhtasari

•Kajala alizawadiwa simu hiyo kali yenye gharama kubwa sana siku ya Jumatatu na mchumba wake Harmonize.

•Nchini Tanzania simu hiyo inawagharimu wateja kati ya Tsh2.5m na Tsh 3m.

Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Muigizaji Fridah Kajala Masanja ni mmiliki mpya wa simu mpya zaidi ya iPhone 14 iliyozinduliwa sokoni siku chache zilizopita.

Kajala alizawadiwa simu hiyo kali yenye gharama kubwa sana siku ya Jumatatu na mchumba wake Harmonize.

Alitangaza kuhusu hilo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo alichapisha video fupi inayoonyesha akiwa ameshika simu hiyo  mpya  ambayo bado haikuwa imetoewa kwenye kijisanduku chake.

"Hommie Wangu katisha!❤ " aliandika chini ya video hiyo.

Aliambatanisha video hiyo na wimbo wa Harmonize 'Deka' ambao anazungumzia wanaume kuwazawadia wapenzi wao.

Majina 'Hommie' na 'bro' ni majina ambayo wanandoa hao wawili mashuhuri huitana mara kwa mara. Ni wazi kuwa Kajala alikuwa akimzungumzia mchumba wake kwa kusema 'Hommie wangu katisha'

Image: INSTAGRAM// KAJALA FRIDA

Simu ya iPhone 14 ambayo ndiyo muundo mpya zaidi wa simu za Apple ilizinduliwa mnamo Septemba 16 na kuwekwa sokoni. Wapenzi wa simu za hizo zinazotumia IOS walianza kuziagiza kutoka Septemba 9.

Kwa sasa iPhone14  inauzwa kati ya shilingi 200,000 na 300,000 nchini Kenya kulingana na soko na uwezo wa kubeba wa simu. Nchini Tanzania simu hiyo inawagharimu wateja kati ya Tsh2.5m na Tsh 3m.

Hii sio zawadi ya kwanza ya gharama kubwa ambayo Kajala amepokea kutoka kwa staa huyo wa Bongo. Mwaka huu pekee Harmonize ametumia mamilioni ya pesa kumfurahisha mchumba wake kwa zawadi ghali.

Magari, mikufu, pete ni baadhi tu ya vitu ambavyo mwanzilishi huyo wa Kondegang amemnunulia mpenziwe tangu mwezi Aprili ambapo alianzilisha juhudi za kuomba msamaha na kufufua mahusiano yao.