"Nakupenda pacha wangu!" Diamond amsherehekea mwanawe na Tanasha Donna

Wengine waliomsherehekea NJ ni pamoja na Zuchu, Mama Dangote na Esma Platnumz.

Muhtasari

•Huku akimsherehea mwanawe kwenye Instagram, Diamond alimtaja kama pacha wake kutokana na kufanana kwao sana.

•"NJ ni mvulana mzuri," Zuchu alisema.

Diamond na Naseeb Juniour
Diamond na Naseeb Juniour
Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo, Diamond Platnumz ameonyesha upendo kwa mtoto wake wa mwisho anayejulikana, Naseeb Juniour.

Naseeb Junior ambaye alizaliwa Oktoba 2, 2019 ni mtoto wa Diamond na aliyekuwa mpenzi wake Tanasha Donna. Wazazi wenza hao walikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa muda hadi mapema 2020 walipotengana.

Huku akimsherehea mwanawe kwenye Instagram, Diamond alimtaja kama pacha wake kutokana na kufanana kwao sana.

"Nakupenda pacha wangu!❤" aliandika chini ya picha mbili za mwanawe alizopakia Jumamosi kwenye ukurasa wake.

Wengine waliomsherehea Naseeb Junior ni pamoja na anayedaiwa kuwa mpenzi wa sasa wa bosi huyo wa WCB, Zuchu, mama yake Mama Dangote, dadake Esma Platnumz na aliyekuwa mpenziwe Harmonize, Jacque Wolper.

"NJ ni mvulana mzuri," Zuchu alisema.

Esma alisema, "Pacha wake mtu!"

Naseeb Junior alizaliwa miezi michache kabla ya wazazi wake kutengana. Tanasha alibaki kumlea mtoto huyo lakini inaaminika kuwa Diamond bado ni sehemu ya malezi kwani wawili hao kwa sasa ni wanashirikiana kulea.

Mwezi Juni wakati staa huyo wa Bongo alipozuru Kenya alifika nyumbani kwa Tanasha na kufurahia muda na mwanawe.

Msanii huyo alipakia video zilizoonyesha akifurahia muda na Naseeb Junior huku wakichapa stori kama watu waliozoeana kwa muda mrefu. Pia walionekana wakicheza na vinyago huku wakishiriki mazungumzo mazuri kwa Kiingereza.

Video nyingine ilimuonyesha Diamond akiwa amemshika mwanawe huku wakijirekodi kutumia kamera ya selfie.

"Mvulana mzuri aje.. Tabasamu N.J," Simba alisikika akimwambia Naseeb Juniour kwenye video hiyo.

Hapo awali Tanasha  alisema hangependa mwanawe awe mwananamuziki kama yeye na mzazi mwenzake Diamond Platnumz. Alisema badala yake angependa mtoto huyo wao wa pekee awe mwanaspoti.

Alieleza kuwa katika siku za usoni angependa sana mtoto huyo wake wa pekee ajihusishe na michezo kama vile soka badala ya muziki.

"Nahisi kama kuna uwezekano. Mama yake ni mwimbaji na baba yake ni mwimbaji. Kuna uwezekano mkubwa wa yeye kufuata njia hiyo, Mungu pekee ndiye ajuaye. Ingekuwa kwa matakwa yangu, ningemtaka awe mwanasoka," Tanasha alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond alibainisha kuwa kimsingi, wanamichezo huwa na nidhamu sana tofauti na wanamuziki.

"Najua watu wanaojihusisha na michezo wana nidhamu sana. Wanaamka mapema, wanafanya mazoezi, wanakimbia, hawanywi pombe kwa sababu kuna vipimo vinavyofanywa kila wakati. Ingekuwa juu yangu, ningetaka hivyo kwa sababu tasnia hii ya muziki inakuja na mengi. Kuna siasa nyingi nyuma yake," Alisema.

Aliongeza "Kuna mengi ambayo huendelea katika tasnia ya muziki. Ukiwa una ushawishi na uko na pesa nyingi, unaweza kuendesha mambo mengi. Ndivyo hukuwa kwenye tasnia nyingi. Hata hivyo naamini kila tasnia huja na mazuri yake na mabaya yake. Hata michezo huwa na upande wake mbaya," 

Tanasha hata hivyo alidokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mwanawe huyo kufuata nyayo zake na Diamond.

Aliweka wazi kuwa ikitokea Naseeb awe mwanamuziki basi hatasita kuunga mkono taaluma yake na kumsaidia kuikuza.