Zari na Diamond wakiri kupendana, wasisitiza familia ipo imara

Staa huyo wa Bongo alimhakikishia bintiye kuwa anampenda Zari pekee na hana mchumba mwingine.

Muhtasari

•Wapenzi hao wa zamani walikiri kupendana katika kikao na watoto wao wakati Diamond alipotembelea familia hiyo yake nchini Afrika Kusini.

•Diamond alimtetea mpenzi huyo wake wa zamani kwa watoto wao na kuwahakikishia kuwa familia bado ipo imara.

Zari Hassan na Diamond Platnumz
Zari Hassan na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM// TIFFAH DANGOTE

Staa wa Bongo Diamond Platnumz na mzazi mwenzake Zari Hassan wamedokeza kuwa bado wanapendana licha ya kutengana miaka kadhaa iliyopita.

Wapenzi hao wa zamani walikiri kupendana katika kikao na watoto wao wakati Diamond alipotembelea familia hiyo yake nchini Afrika Kusini.

Katika kikao hicho, Tiffah na Prince Nillan walimlaumu mama yao kwa kusababisha kuvunjika kwa mahusiano yake na Diamond. Pia walikana madai ya mwanasoshalaiti huyo kuwa familia yao ilisambaratika baada ya Diamond kupata mpenzi mwingine.

"Je, niko na mpenzi mwingine?" Diamond alimuuliza bintiye ambaye alijibu kwa  "HAPANA!" bila kusitasita.

Bosi huyo wa WCB aliendelea kumhakikishia bintiye kuwa anampenda Zari pekee na hana mchumba mwingine.

"Nilikwambia nampenda mtu mmoja tu, nampenda nani? Mama T (Zari) sina nguvu ya mwingine," alisema.

Tayari Tiffah alikuwa ashaanza kutoa malalamiko mengine dhidi ya mamake Zari kabla yake kuingilia kati na kumwambia "Nampenda papa pia, nilikwambia."

Baada ya wazazi wao kukiri kupendana, Tiffah aliendelea kulalamika kuhusu mama yake kupata mpenzi mwingine.

Pamoja na kakake Nillan, pia alikanusha madai kuwa baba yao yuko katika mahusiano na mwanamke mwingine.

"Lakini sasa mama yuko na mtu mwingine, nasema  ukweli," Tiffah alimwambia Diamond.

Mwimbaji huyo alijifanya kushtuka sana kusikia kuwa mzazi huyo mwenzake anachumbiana na mwanaume mwingine.

Zari ambaye alikuwa akifuatilia kwa makini wakati watoto wake wakiibua madai mazito mazito dhidi yake alionekana kushangazwa sana na jinsi walivyogeuza kidole cha lawana kutoka kwa mpenzi huyo wake wa zamani na kuelekeza kwake.

Tiffah aliendelea kumlalamikia mamake kwa kuvunja familia huku akimkosoa kwa kujitosa kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

"Kwa nini uliivunja familia? Uko na mtu mwingine, unatumia muda wako naye, huna wakati na familia, hatumii wakati wako na baba!" alimlalamikia mamake.

Alilalamika sana kuhusu hatua ya mamake kutumia muda mwingi na mpenzi wake mpya siku za wikendi badala ya kuwa na baba yao.

Diamond hata hivyo alimtetea mpenzi huyo wake wa zamani kwa watoto wao na kuwahakikishia kuwa familia bado ipo imara.

"Hatukuvunja familia. Familia bado iko imara," aliwaambia.