Huku Harmonize akidaiwa kumpa ujauzito Kajala, aliyekuwa mpenziwe azama kwenye dimbwi la mahaba

Briana alidokeza kuwa tayari yupo kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

Muhtasari

•Harmonize alitangaza kutengana na mrembo huyo wa Australia mwezi Machi kabla ya kuanza harakati za kufufua uhusiano wake na Kajala.

•Briana alichapisha video inayoonyesha mkono wa mwanamume mweusi akimpapasa kidevu kwa njia ya kimahaba

Harmonize na Briana
Harmonize na Briana
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Mwanamitindo Briana Jai amedokeza mahusiano mengine, takriban miezi minane baada ya kutengana na staa wa Bongo Harmonize.

Harmonize alitangaza kutengana na mrembo huyo wa Australia mwezi Machi kabla ya kuanza harakati za kufufua uhusiano wake na Kajala.

Wakati huo, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alieleza kuwa aliachana na Briana kufuatia sababu kadhaa ikiwemo kuwa bado alikuwa na hisia za mapenzi kwa muigizaji Kajala, ambaye alikuwa ametengana naye wakati huo.

“Kuhusu Briana sina Tatizo nae kabisa, ni mtu mzuri ila hatuko pamoja, sababu nambari moja, nilimwambia nimetengana na mtu bila kugomabana na nampenda sana. Sasa sina uhakika kama nimemove on, lolote linaweza kutokea maana," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram mwishoni mwa mwezi Machi.

Pia alifichua kuwa aliachana na mwanamitindo huyo kutokana na tofauti za mawazo. Alisema walitofautiana kuhusu nchi gani ya wao kuishi huku kila mmoja akipendelea kukaa katika nchi yake ya kuzaliwa.

Huku akithibitisha kutengana kwao, Briana alimtakia kila la heri mwimbaji huyo na kufichua kwamba alikuwa amerejea  nyumbani kwao Australia.

“Kwa sasa nipo nyumbani Australia. ni kweli tumeachana na Harmonize namtakia kila laheri maishani mwake. Nashukuru kwa wale wote walionisupport nilipokuwa Tanzania nawapenada wote na kwa hayo nitarudi kuwatembelea tena. Inshallah,”  alisema.

Tangu wakati huo, Briana amesalia kimya kuhusu uhusiano wake na msanii huyo na maendeleo ya maisha yake ya mapenzi.

Katika chapisho la Instastori la hivi punde hata hivyo, alidokeza kuwa tayari yupo kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

Mwanamitindo huyo alichapisha video inayoonyesha mkono wa mwanamume mweusi akimpapasa kidevu kwa njia ya kimahaba. Briana alionekana akitabasamu huku mwanaume huyo asiyetambulishwa akiendelea kumpapasa.

Image: INSTAGRAM// BRIANA JAI

Haya yanajiri huku kukiwa na tetesi kuwa Harmonize na mchumba wake wa sasa Kajala wanatarajia mtoto wao wa kwanza.

Siku chache zilizopita wawili hao waliongeza uzito kwenye tetesi hizo kwa kuchapisha picha ya Harmonize akipapasa tumbo la mwanamke mjamzito na kuambatanisha na jumbe za kudokeza wanatarajia mtoto.

Madai hayo ya ujauzito hata hivyo yametiliwa shaka huku ikidaiwa Kajala amekuwa akiugua tu kwa muda.