Harmonize awakejeli wapenzi wake wa zamani Wolper, Sarah na Briana

Bosi huyo wa Kondegang ametumia wimbo 'My Way' kuwashambulia wapenzi wake wa zamani.

Muhtasari

•Harmonize anazipuuza pesa za Sarah Michelloti ambaye alichumbiana naye kwa muda na kusema ni karatasi tu.

•Anadokeza kuwa bado alikuwa mgeni wa mapenzi wakati akichumbiana na Wolper na alitengana naye kufuatia hofu ya kushindana na mabwenyenye.

Harmonize na mchumba wake Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Bosi wa Konde Music Worldwide Harmonize ameratibiwa kuachia albamu yake mpya  'Made for Us' siku ya Ijumaa.

Staa huyo tayari amefichua majina ya nyimbo 14  zilizo katika albamu hiyo inayosubiriwa sana na mashabiki wa Bongo.

Nyimbo katika albamu hiyo ni pamoja na;- Mwenyewe, My Way, Leave me alone, Wote, Nitaubeba, Utanikumbuka, I miss you, Die, The way you are, Miss Bantu, Best Friend, Deka, Too Much na Amelowa.

Tayari ameachia nyimbo kadhaa katika albamu hiyo, baadhi sauti pekee  huku zingine akiwa ameachia video na sauti. 

Katika wimbo 'My Way', Harmonize kimsingi anawashambulia wapenzi wake watatu wa zamani  na kumsifia mchumba wake wa sasa Kajala Masanja. Anadokeza kuwa bado alikuwa mgeni wa mapenzi wakati akichumbiana na Wolper na alitengana naye kufuatia hofu ya kushindana na mabwenyenye.

"Ile mwanzo mwanzo nalijua kopa, moyo ukadondoka kwa Wolper. Ningali bado mdogo nikaogopa, Hivi nitawezaje kushindana na vibopa,"  anasema Harmonize katika kifungu cha Wimbo huo wa dakika mbili.

Anaendelea kuzipuuza pesa za mwanamitindo Sarah Michelloti ambaye alichumbiana naye kwa muda na kusema ni karatasi tu.

"Nikasema hasara roho pesa makaratasi , si nikampa Sarah roho kulipiza kisasi. Labda niseme ni mambo ya ujana, ama pengine nyota zilipishana. Kila siku tukawa  tunagombana, hapa kati kabla hajaja Briana," aliimba.

Harmonize alisisitiza kuwa mapenzi yake na Sarah yalikuwa ya kweli na kudai waliafikia kutengana bila kugombana.

Anaendelea kukiri kwamba alikumbwa na msongo wa mawazo wakati ambapo uvumi mwingi ulienezwa kumhusu.

"Haters walidhani nitajinyonga. Hello now it's true am stronger. You don't teach my how to live. Don't tell me how to live my life," anaimba.

Inatafsiri: (Wenye chuki walidhani nitajinyonga. Halo sasa ni kweli nina nguvu zaidi. Hunifundishi jinsi ya kuishi. Usiniambie jinsi ya kuishi maisha yangu.)

Katika wimbo huo, bosi huyo wa Kondegang anawaarifu watu kuwa anafanya mambo yake jinsi atakavyo.