Jeshi vs Simba: Jinsi Diamond alivyopandisha ugomvi na Harmonize

Mastaa hao wa Bongo wamekuwa wakizozana tangu Harmonize alipogura WCB mwakani 2019.

Muhtasari

•Wawili hao wamekuwa wakiendeleza uhasama wao aidha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, hivi majuzi ikiwa ni kuhusu uzinduzi wa Albamu.

•Lebo ya Diamond ya WCB pia ilifichua mipango ya kuzindua EP ya msanii wake Mbosso Khan.

Harmonize na Diamond
Image: INSTAGRAM

Mvutano kati ya mastaa wawili wakuu wa Bongo, Harmonize na Diamond Platnumz hauna dalili zozote za kufika kikomo hivi karibuni.

Kwa muda mrefu, wawili hao ambao waliwahi kufanya kazi pamoja katika siku za nyuma wameendeleza uhasama wao aidha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, hivi majuzi ikiwa ni kuhusu uzinduzi wa Albamu.

Wikendi iliyopita, Konde Boy alitangaza kwamba ataachia Albamu yake mpya 'Made for Us' kuelekea mwishoni mwa mwezi huu.

"MADE FOR US 28/10/22," alitangaza kwenye Instagram.

Bosi huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide pia alifichua orodha ya nyimbo kumi na nne katika albamu yake mpya.

Nyimbo katika albamu hiyo inayosubiriwa sana na mashabiki wa Bongo ni pamoja na;- Mwenyewe, My Way, Leave me alone, Wote, Nitaubeba, Utanikumbuka, I miss you, Die, The way you are, Miss Bantu, Best Friend, Deka, Too Much na Amelowa.

Harmonize aliweka wazi kuwa hana nia ya kuifanyia matangazo Albamu ya 'Made for Us' kwani tayari ashafanya kila kitu studioni.

"Hakuna mkutano na waandishi wa habari, hakuna ziara ya vyombo vya habari, hakuna mabango, hakuna karamu ya kusikiliza. Nimefanya kila kitu studio kwa hivyo hakuna haja ya hype. Chapisho moja labda. Nilitengeneza hii kwa ajili yenu Afrika Mashariki na kila mtu anayezungumza Kiswahili duniani," alisema kwenye Instastori.

Muda mfupi baada ya mchumba huyo wa muigizaji Kajala Masanja kutangaza kuwa ataachia Albamu yake mwishoni mwa wiki hii, lebo ya Diamond ya WCB pia ilifichua mipango ya kuzindua EP ya msanii wake Mbosso Khan.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond alitangaza kuwa EP ya msanii huyo wake itazinduliwa rasmi siku ya Alhamisi.

"Ndio!! Mbosso EP Launch! Alhamisi hii Oct 27 katika hoteli ya Barra Beach! Ushauri wangu, we jitahidi tu ufanye ufanyavyo upate mualiko maana dah utapitwa na mengi sana," Diamond alisema siku ya Jumanne.

Bosi huyo wa alisema kuwa kamati ya EP ya msanii huyo wake iliafikia kutangaza rasmi jina la EP hiyo siku ya Jumatano.

"Kamati imesema: Kesho jina la EP ya Mbosso Khan litatangazwa Rasmi! #KamatiImesema," alisema kwenye Twitter.

Harmonize alivunja uhusiano wake na Diamond na kuondoka WCB Wasafi mwishoni mwa 2019. Tangu wakati huo amefanya miradi kadhaa akiwa peke yake na hata kuanzisha lebo yake ya muziki, Konde Music Worlwide