Nilijilipia mahari baada ya kuchumbiana kwa miaka 9 - Mwanamke, 34, asimulia

Mara ya kwanza mumewe alipinga wazo hilo ila baadae akakubali kwa sababu mwanamke huyo kipato chake kilikuwa juu kumliko.

Muhtasari

• Simulizi yake ilizua mjadala mitandaoni huku wengine wakisema mila za Kiafrika hazirihusu hivyo na wengine wakisema mchakato wa ndoa ni kusaidiana.

Image: THE STAR

Mwanamke mmoja aliyegonga vichwa vya habari baada ya simulizi yake kuvujishwa kuwa alitumia pesa zake na gharama nyingine zake mwenyewe kusimamia ndoa yake hadi kulipa mahari mwenyewe.

Mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 34 kwa jina Zuku hakuwa mtu hivi hivi bali ni msomi aliyehitimu na sifa kadhaa za uzuri na ulimbwende.

Wazazi wake baada ya kujitutumua na kumsomesha, walikuwa na matumaini ya juu kupata angalau kufutwa machozi kidogo kwa kulipwa mahari ya kiwango cha aina yake na mwanaume aliyemchumbia binti yao.

Lakini hali iligeuka wakati waligundua kuwa binti yao ndiye aliyejitolea kuzama mkobani na kujilipia mahari.

Akisimulia kisa hicho kwenye News24, Zuku alisema yeye binafsi alikuja na wazo la kulipa mahari kwa niaba ya mpenzi wake.

“Ikiwa mtu angeniambia kuwa katika umri wa miaka 34, ningekuwa nalipa mahari yangu mwenyewe, ningecheka. Lakini ndio, ilifanyika - nililipa mahari yangu mwenyewe kikamilifu, na sitasema uwongo; mwanzoni, niliaibika,” Zuku aliiambia NEWS24.

Alizidi kumwaga ubuyu akitetea hatua yake kuwa si ya kukurupuka bali alikuwa amekaa na huyo mchumba wake kwa miaka kadhaa kabla ya kuafikia uamuzi wa kumsaidia kutekeleza jukumu hilo ambalo katika mila na destruri za Kiafrika ni jukumu la mwanaume.

Walichumbiana kwa miaka 9 na mwanzoni alipomwambia mchumba wake lengo lake la kumsaidia kulipa mahari, alidinda ila mwisho wa siku akakubali kwani hakuna mkate mgumu mbele ya chai siku zote!

“Mume wangu hakuunga mkono wazo hilo na alikataa pendekezo langu, lakini lilikuwa na maana sana. Familia yake ingelipa pesa nyingi sana kwa sherehe za harusi na kuipa familia yangu zawadi. Pia nilipata pesa nyingi kuliko yeye na nilikuwa na uwezo wa kupata pesa za mahari. Wakati huo, alijiona kuwa mnyonge lakini kwa mtazamo wa nyuma; ilikuwa na maana zaidi ya kifedha kwa sisi sote na maisha ambayo tulikuwa karibu kujenga pamoja.