Akothee ajigamba kuhusu gauni lake ghali la harusi “ni bei ya gari la ndoto yako”

Mwimbaji huyo alifichua kuwa yeye na mpenzi wake watafunga pingu za maisha mwezi ujao.

Muhtasari

•"Nilisema ndio kwa gauni. Sasa imebaki ndio kwa mpenzi wa maisha yangu," mwanamuziki huyo alisema.

•Akothee aliwasili nchini Uswizi siku ya Jumapili asubuhi ambapo alikutana na mpenzi wake mzungu.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee hatimaye amepata gauni kwa ajili ya harusi yake ijayo.

Siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto watano ambaye kwa sasa yuko ziarani katika jiji la Zurich, nchini Switzerland aliweka wazi kuwa tayari amekubali gauni ambalo mchumba wake Bw Schwiezer alimnunulia.

"Nilisema ndio kwa gauni. Sasa imebaki ndio kwa mpenzi wa maisha yangu," mwanamuziki huyo alisema kwenye Instagram.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alidokeza kuwa gauni hilo Iiligharimu pesa nyingi, za kutosha kununua gari la kifahari.

"Gauni langu la harusi ni bei ya gari la ndoto yako. Imekaomomilika," alitangaza.

Akothee aliwasili nchini Uswizi siku ya Jumapili asubuhi ambapo alikutana na mpenzi wake mzungu ambaye amebatiza jina Bw Omosh.

Wiki iliyopita, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa yeye na mpenzi wake mzungu watafunga pingu za maisha mwezi ujao.

"Siwezi @misteromosh .. Ni April 10," Akothee ambaye alionekana kuzidiwa na hisia ya furaha alisema kwenye Instagram.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliambatanisha tangazo hilo na video za bustani nzuri ambapo alidokeza kuwa harusi yake na Bwana Omosh itafanyika. Alikuwa ameenda kukagua matayarisho yanavyoendelea.

"Katika ukaguzi wa eneo la siku ya harusi yangu, mume wangu aliagiza bwawa la maji," Akothee aliandika.

Baadaye, alifichua kuwa anaelekea Ulaya kwa minajili ya kununua gauni linalokidhi viwango ambavyo mchumba wake anataka.

"Ninaenda katika jiji la mapenzi kwa gauni langu la harusi. Kwa hivyo unamaanisha hakuna gauni nchini Kenya," alisema kupitia Instagram.

Mwanamuziki huyo alidokeza kwamba hakufanikiwa kupata gauni zuri ambayo mpenzi wake anataka humu nchini Kenya.

Bw Schwiezer almaarufu Bw Omosh alimvisha Akothee pete ya uchumba katikati mwa mwaka jana, miezi michache tu baada ya mahusiano yao kujulikana wazi. Mwanamuziki huyo alijitosa kwenye mahusiano na Bw Omosh baada ya kutengana na aliyekuwa meneja wake, Nelly Oaks mwishoni mwa mwaka 2021.