Akothee kuolewa rasmi na mpenziwe mzungu, afichua tarehe na mipango ya harusi

Ndoa ya kwanza ya mwanamuziki huyo iligharimu Ksh 2,500.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano alionyesha kwamba mipango ya siku hiyo kubwa katika maisha yake inaendelea.

•Akothee alithibitisha kuwa ndoa yake ya kwanza ilivunjwa rasmi mnamo Mei  22, 2011 baada ya kesi ya talaka kuwasilishwa  2007. 

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee amefichua kwamba anapanga kufanya harusi na mchumba wake anayetambulisha kama Bwana Omosh.

Siku ya Ijumaa, mama huyo wa watoto watano alionyesha kwamba mipango ya siku hiyo kubwa katika maisha yake inaendelea.

Alitangaza kuwa yeye na mchumba huyo wake mzungu watafunga pingu za maisha mnamo Aprili 10, mwaka huu.

"Siwezi @misteromosh .. Ni April 10," Akothee ambaye alionekana kuzidiwa na hisia ya furaha akisema kwenye Instagram.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliambatanisha ujumbe wake na video za bustani nzuri ambapo alidokeza kuwa harusi yake na Bwana Omosh itafanyika. Alikuwa ameenda kukagua matayarisho yanavyoendelea.

"Katika ukaguzi wa eneo la siku ya harusi yangu, mume wangu aliagiza bwawa la maji," Akothee aliandika.

Katika video alizochapisha, bustani la harusi hiyo ijayo lilionekana safi, na maua mazuri pamoja na nyasi zilizokatwa vizuri.

Harusi ya mwanamuziki huyo inakuja takriban miezi minne baada ya dada yake mdogo, Cebbie Koks, ambaye hana uhusiano mzuri naye, kufunga pingu za maisha na mume wake Steve Ogolla katika harusi ya kitamaduni.

Wawili hao walifanya harusi ya kitamaduni katika moja ya mandhari safi eneo la Nyanza ambapo watu wanafamilia, marafiki na watu kadhaa maarufu walihudhuria  hafla hiyo ya kupendeza kweli kweli.

Hapo awali, mama huyo wa watoto watano aliwahi kufichua kuwa harusi yake ya kwanza na aliyekuwa mumewe, Jared Okello.

Oktoba mwaka jana, alichapisha picha iliyomuonyesha na familia yake mnamo siku ya harusi iliyofanyika miongo miwili iliyopita.

"Harusi yetu iliyogharimu Sh2500 (Imara) Wanandoa wapya waliofunga ndoa wakionyesha malengo ya wanandoa katika kanisa la Awendo SDA mnamo tarehe 6 Julai, 2002," alisema chini ya picha hizo.

Aidha, alithibitisha kuwa ndoa yake na baba huyo ya binti zake watatu ilivunjwa rasmi mnamo Mei  22, 2011 baada ya kesi ya talaka kuwasilishwa mwaka wa 2007. Hi ni baada ya kuwa kwenye ndoa rasmi kwa takriban miaka mitano.

Wakati huohuo, mwimbaji huyo wa miaka 43 alitangaza kwamba anahisi kama maisha yake yamekamilika baada ya kukutana na Shweizer na kusema yuko tayari kutulia kwenye ndoa naye na kuwa mke mtiifu.

"Sikujua kijiji changu kingeweza kuwa Paradiso. Mfalme alikuwa akikosekana. Sasa naweza kusema maisha yangu yamekamilika na niko tayari kutulia, niko tayari kuwa mke mtiifu," Akothee alisema