“Upande mmoja ulikufa kabisa!” Akothee afunguka kuhusu tatizo la kutisha alilopambana nalo

Mwimbaji huyo alisema tatizo hilo lilikithiri hadi akalazimika kufanyiwa upasuaji.

Muhtasari

•Akothee alifichua kwamba kuna kitu ambacho kilikuwa kikiathiri kichwa chake na kumfanya ajisikie kuishiwa nguvu.

•Akothee alieleza kwamba tatizo hilo lilimsababishia matatizo ya kupumua na kufa ganzi katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amefunguka kuhusu tatizo la kutisha la kisaikolojia ambalo alipambana nalo na kufanikiwa kutoka akiwa hai katika siku za nyuma.

Akizungumza kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto watano alifichua kwamba kuna kitu ambacho kilikuwa kikiathiri kichwa chake na kumfanya ajisikie kuishiwa nguvu.

"Nilijawa na milipuko na hisia zisizodhibitiwa. Nilikuwa nikipambana na kuwa mimi bila kumuudhi mtu yeyote, nilikuwa nikijitahidi kukubali kile ambacho umaarufu unanitupia. Nilikuwa nikikubali kwamba wakati fulani itabidi niwache mengi kabisa," Alisema.

Aliongeza, "Nilikuwa nikihangaika kuwaacha watu wengine watoke kwenye maisha yangu bila kuwaumiza na kuwapenda kutoka mbali, ndio nilikuwa nikipambana na kukubali kwamba mara nyingi nitalazimika kufanya uzazi wa mitandaoni na niachiwe majumba yote pamoja na mbwa na ndege.

Nilikuwa nikipambana na kutojisikia vibaya ninapokutana na mashabiki wangu ambao walifurahi kuniona na sikuwa katika hali ya kumuona mtu yeyote akiwa na furaha, wakati fulani ilionekana kama usumbufu, simu zilikuwa zinakera na niliona watu wengi wakinikujia wala sio kuja kwa ajili yangu. Nilikuwa nikijitahidi kupata nafasi yangu. Nilikaribia kukata tamaa, nilihisi kuzidiwa na mengi."

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alieleza kwamba tatizo hilo lilimsababishia matatizo ya kupumua haswa nyakati za usiku na kufa ganzi katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

"Wakati fulani sikuweza kupumua usiku ghafla tu, nilimwomba mpenzi wangu afungue madirisha, nilikuwa nikikosa hewa, Kuanzia usiku mmoja hadi mwingine, niliamka huku upande wangu wa kushoto ukiwa umekufa ganzi, ganzi ilienea kutoka shingoni hadi mguuni.

Wakati mmoja niliamka huku upande mmoja ukiwa umekufa kabisa. Niliogopa na kutoka siku moja hadi nyingine, nilipoteza nguvu kwenye mkono wangu wa kushoto, nisiweze hata kuinua chochote," alisimulia.

Alieleza kuwa tatizo hilo liliendelea kuwa baya zaidi hadi akalazimika kufanyiwa upasuaji. Baada ya kutembelea hospitali  mara kadhaa amesema alihama kwake na kuenda kwa dada yake kwa lengo la kupata afueni kikamilifu.

Alisema kwamba tatizo alilokuwa nalo lilimmaliza nguvu na kumfanya awe na hisia kali kiasi cha kupatiwa dawa za kutuliza mawazo.

"Hisia ziliongezeka maradufu na mashambulizi mabaya ya hofu🤔 Kuanzia siku moja hadi nyingine nilihitaji vidonge vya kulala vyenye nguvu zaidi, Siku moja nilimuomba daktari anidunge tu dawa ya usingizi  yenye nguvu ili nilaleeeee," alisema.

Mwaka wa 2021, mwanamuziki huyo alilazwa hospitalini mara kadhaa baada ya kushambuliwa na maradhi ambayo hakufichua.