Akothee asimulia bintiye alivyoathirika kufuatia talaka yake, alivyohangaika kumtafutia baba

"Majibu yake yalikuwa yanauma kwa hivyo sikuweza kuwaambia watoto hataki kuongea nasi," alisema.

Muhtasari

•Akothee alifichua kuwa Makadia alikuwa na umri wa miaka minne tu alipotalikiana na aliyekuwa mumewe, Jared Okello.

•Mwimbaji huyo alidai kuwa mzazi mwenzake wa pili alikataa kuwakubali mabinti wake watatu kama wanawe.

Akothee na binti yake Fancy Makadia
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee amefunguka kuhusu matatizo ambayo alipitia na bintiye mdogo Fancy Makadia alikiwa mdogo.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram siku ya Ijumaa, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa Makadia alikuwa na umri wa miaka minne tu alipotalikiana na aliyekuwa mume wake wa kwanza, Jared Okello.

Akothee alisema bintiye aliathiriwa sana na talaka hiyo kwani alikosa kuelewa kwa nini hangeweza kumuona babake wala kuzungumza naye.

"Mara kadhaa ilinibidi ninunue sim card mpya, niizime na kujifanya nampigia simu baba yake, nilidanganya sana kuficha maumivu," Akothee alisimulia.

Mwimbaji huyo mkongwe alifichua kuwa baada ya mume huyo wake wa zamani kupata familia nyingine, alimdanganya Makadia kwamba alikuwa amesafiri kuenda nje ya nchi kwani hakutaka kumsumbua Bw Jared kwa simu.

"Majibu yake (Bw Jared) yalikuwa yanauma kwa hivyo sikuweza kuwaambia watoto hataki kuongea nasi," alisema.

Akothee aliendelea kufichua kwamba wakati alipojitosa kwenye ndoa nyingine na mwanaume mzungu kutoka Switzerland, Papa Ojwang, mzazi huyo mwenzake wa pili alikataa kuwakubali mabinti wake watatu kama wanawe.

Alidai kwamba Papa Ojwang alimtaka tu mtoto wake halisi, Prince Ojwang' na hakutaka kamwe kuwawajibikia watoto wake wengine kutoka ndoa ya awali ambao ni Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia.

"Nilipokutana na DOMINIQUE, babake Oyoo alikumbatia watoto wangu na Fancy Makadia akapata BABA. Alikuwa, na bado ni mtoto kipenzi cha Dominic kutoka kwa watoto wangu. Tukitaka kitu kutoka kwa Baba, tulikuwa tunatuma Makadia kabla Oyoo hajazaliwa," alisema mwanamuziki huyo.

Akothee aliweka wazi kuwa Bw Dominique alimsaidia kumhamisha shule binti yake Makadia kumpeleka shule ya kifahari.

Baadaye, Makadia alihamia nchini Ufaransa ambako aliendeleza masomo yake hadi kuhitimu chuo kikuu mwaka jana.