Shangwe na nderemo huku Mulamwah, mkewe na mwanawe wakitua nyumbani kwa gari lake jipya

Vijana walionekana wakikimbia mbele ya gari la Mulamwah, wengine wakifuata nyuma na pembeni huku wengine wakifuata kwa pikipiki.

Muhtasari

•Mulamwah na familia yake walikaribishwa kwa shangwe na nderemo walipozuru nyumbani kwao Kitale, mnamo siku ya Jumanne.

•Ruth K alionekana kufurahia mapokezi hayo mazuri na akawahakikishia mashabiki kwamba angeshiriki video ya kina kuihusu tukio hilo.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji mashuhuri wa Kenya David Oyando almaarufu Mulamwah, mpenzi wake Ruth K na mwana wao Oyando Jr walikaribishwa kwa shangwe na nderemo walipozuru nyumbani kwao Kitale, kaunti ya Trans Nzoia mnamo siku ya Jumanne.

Baba huyo wa watoto wawili alichapisha video za wakazi kadhaa, hasa vijana wakiwa na pikipiki wakiwakaribisha kwa shangwe tele huku wakiwa wamebeba matawi wakati alipokuwa akilindesha nyumbani gari lake jipya aina ya Mercedes lililokuwa limebeba familia yake.

Katika video hiyo, baadhi ya vijana walionekana wakikimbia mbele ya gari la Mulamwah, wengine wakifuata nyuma na pembeni huku wengine wakifuata kwa pikipiki huku wakipiga honi.

“Kitale!” Mulamwah aliandika chini ya video hizo na kuisindikiza kwa emoji ya moyo ili kuashiria upendo.

Mpenzi wake, Ruth K pia alionekana kufurahia mapokezi hayo mazuri na akawahakikishia mashabiki wake kwamba angeshiriki video ya kina kuihusu tukio hilo.

Hapo awali, mchekeshaji huyo alikuwa amedokeza kwamba angempeleka mtoto wake mdogo, Oyando Jr nyumbani.

"Kalamwa ufike nyumbani sasa," alisema wikendi na kuambatanisha ujumbe huo na picha yake, mpenziwe na mwanawe katika uwanja wa ndege.

Kuelekea mwishoni mwa mwezi Machi, Mulamwah alifichua habari za fanikio lake kubwa la kununua gari aina ya Mercedes Benz E250.

 Wakati akitoa tangazo hilo, mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alimshukuru Mungu, familia yake na mashabiki kwa jukumu muhimu walilocheza katika mafanikio hayo.

“MUNGU ALIFANYA 💪🙏 mmiliki gari mwenye fahari 💯 mercedes BENZ E250 innit . kila mara tembea polepole lakini, sogea ipasavyo 💯. namshukuru Mungu kwa baraka zote maishani, wacha tuanzie ka life apa . shukrani kwa familia, mashabiki na marafiki kwa usaidizi wenu na maombi kila mara,” Mulamwah alisema.

Baba wa watoto wawili alidokeza kuwa gari hilo sasa litamsaidia mzazi mwenzake Ruth na mtoto wao mdogo kusafiri hadi kliniki kwa urahisi kila inapohitajika.

Pia hakusahau kumshukuru mpenzi wake kwa sapoti ambayo ameendelea kumpa.

 “Kijana cha kitale sasa ni former pedestrian. kalamwah na mama kalamaz clinic wanafika in style sasa . @atruthk asante kwa support daima mamake,” alisema.

Mpenzi wake Ruth K, kwa upande wake alimsherehekea kwa kununua gari hilo maridadi na kumpongeza kwa mafanikio hayo.

"Hongera baba Kalamwah," Ruth K aliandika chini ya video yake akiwa amesimama kando ya gari nyeusi aina ya Mercedes.

Alibainisha kuwa Mulamwah anastahili sana gari hilo akifichua kwamba ilimchukua bidii, maombi na kujitolea kulinunua.

"Matokeo ya uvumilivu, maombi, bidii na kujitolea🎉🎉 hongera baba kalamz @oyando_jnr kwa ushindi huu♥️," aliandika.

Aliongeza, "Hii ni ya thamani ya kusubiri , Nisaidieni kumpongeza mmiliki mpya wa gari mjini🎉♥️anastahili sana. Ninafurahi na kujivunia wewe sana, nakupenda♥️.Road test unanipelek#a wapi🙈😋

Mama huyo wa mvulana mmoja pia hakuweza kuficha jinsi anavyojivunia mpenzi wake.