Diana Marua awahoji watoto Heaven na Mueni Bahati kuhusu wapenzi wao, wajibu

Swali la kipekee zaidi ambalo aliwauliza wasichana hao wawili ni kama wana wapenzi.

Muhtasari

•Pia alitoa ushauri kwa wasichana hao wawili katika mazungumzo hayo aliyochapisha kwenye chaneli yake maarufu ya YouTube.

•Heaven alisema aliogopa mvulana aliyevutiwa naye angewaambia marafiki zake kuhusu uhusiano wao, jambo ambalo hakutaka

akishiriki mazungumzo na Heaven na Mueni Bahati.
Diana akishiriki mazungumzo na Heaven na Mueni Bahati.
Image: YOUTUBE// DIANA MARUA

Mwanavlogu maarufu wa Kenya Diana Marua hivi majuzi alikuwa na mazungumzo ya wazi na bintiye Heaven Bahati na mtoto wa kwanza wa Bahati, Mueni Bahati ambapo aliwauliza maswali kadhaa kuhusiana na maisha yao.

Mama huyo wa watoto watatu pia alitoa ushauri kwa wasichana hao wawili katika mazungumzo hayo ambayo alichapisha kwenye chaneli yake maarufu ya YouTube.

Swali la kipekee zaidi ambalo aliwauliza wasichana hao wawili ni kama wana wapenzi, swali ambalo wote wawili walijibu kwa ujanja.

Heaven ambaye ni mtoto wa kwanza wa Diana alidai kuwa alikuwa amekataa ombi la kuwa mpenzi wa mvulana mmoja kutoka shuleni kwao ambaye pia ni jirani yao.

"Sina mpenzi, lakini S***n alisema anataka niwe rafiki wake wa kike. Lakini nikasema hapana,” Heaven alisema.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka sita alibainisha  kwamba aliogopa kwamba mvulana aliyevutiwa naye angewaambia marafiki zake kuhusu uhusiano wao, jambo ambalo hakutaka.

"Hatunzi siri kamwe," alisema.

Kwa upande wake, Mueni alisema hana mpenzi. Hata hivyo alibaini kuwa kuna mvulana ambaye anamchukulia kama rafiki yake mkubwa.

"Tunacheza naye tu, ni mwanafunzi mwenzangu," Mueni alisema.

Aliweka wazi kuwa hangependa kuwa mpenzi wa mvulana huyo kwani aliogopa wanafunzi wenzake wangeanza kuwazungumzia.

Diana aliweka wazi kuwa yeye hufanya vlog kama hizo na watoto wake ili katika siku zijazo waweze kuangalia nyuma jinsi wametoka mbali.

Pia aliwashauri wasichana hao wawili kujisikia huru kila mara kuzungumza naye kuhusu jambo lolote; ikiwemo kuhusu wavulana, hisia na mambo mengine katika maisha yao.