Wapenzi wa zamani wa Diamond wafurahi na kukumbatiana baada ya kukutana

Wawili hao wamewahi kuchumbiana na Diamond Platnumz katika nyakati tofauti.

Muhtasari

•Whozu alichapisha video iliyowaonyesha wawili ha wakikumbatiana huku wakionekana wenye bashasha tele pamoja. 

•Mkutano wa Mobetto na Sepetu na ushirikiano wao unadhihirisha wazi kwamba kuna uhusiano mzuri sana kati yao.

Diamond Platnumz, Wema Sepetu, Hamisa Mobetto
Image: INSTAGRAM

Muigizaji wa Bongo Wema Sepetu na mwanamitindo Hamisa Mobetto walikutana na kufurahia muda pamoja siku ya Jumatano.

Mpenziwe Wema Sepetu, Whozu alichapisha video iliyowaonyesha wasanii hao wawili wakiwa wanakumbatiana huku wakionekana wenye bashasha tele pamoja. Kwenye video hiyo, walivalia dera zuri na walipendeza sana.

Ingawa hawakutoa maelezo mengi kuhusu mkutano wao, kuna uwezekano mkubwa kwamba Wema alimtembelea Mobetto katika duka lake la nguo la Mobetto Styles kwa ajili ya kumsaidia kutangaza bidhaa zake mitandaoni.

"Mrembo Mrembo. Haya wapendwa wangu, ebu niambieni kati ya haya magauni matatu ya Mobetto Styles ni lipi haswaa linampendeza kipenzi chetu cha Tanzania Wema Sepetu," Hamisa Mobetto aliandika chini ya picha za muigizaji huyo akiwa amevalia magauni matatu tofauti ambazo alipakia kwenye Instagram.

Mama huyo wa watoto wawili anamiliki duka kubwa la mavazi haswa ya kike katika jiji la Dar Es Salaam, nchini Tanzania.

Mkutano wake na Wema Sepetu na ushirikiano wao unadhihirisha wazi kwamba kuna uhusiano mzuri sana kati yao. Wawili hao wamewahi kuchumbiana na staa wa Bongo Diamond Platnumz katika nyakati tofauti.

Mobetto ambaye ndiye wa mwisho kuwa kwenye mahusiano na bosi huyo wa WCB kati ya wawili hao anaaminika kuwa na mtoto wa kiume naye, Dylan Abdul Naseeb. Hata hivyo kumekuwa na mvutano kati ya wawili hao kuhusu mtoto huyo.

Mwaka jana, mwanamitindo huyo alilalamika kwamba Diamond amemtelekeza mtoto wao na kueleza kwamba hajui sababu yake.

Hii ni baada ya mzazi huyo mwenzake kutomsherehekea mvulana huyo mdogo akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

"Kusema ukweli sifahamu kwa nini nadhani hilo swali ni vizuri sana akiulizwa yeye mwenyewe binafsi mi ntakua sina majibu na mi si mtu ambaye anauliza nadhani ni maamuzi tu mtu unaamka tu asubui unaamua," alisema.

Diamond na Wema Sepetu walichumbiana kati ya mwaka wa 2012 na 2014 ila hawakuwahi kupata mtoto pamoja.

Katika mahojiano ya awali, muigizaji huyo aliwahi kumshtumu Diamond kwa kuwa mpenzi mwenye vurugu.