Rayvanny afichua sababu ya kutumia mamilioni kurekodi video moja katika miji mitano

"Yote ni kuhusu muziki mzuri na video nzuri kwa mashabiki wangu," alisema

Muhtasari

•Rayvanny aliweka wazi kwamba shughuli ya kurekodi video yake ijayo imemgharimu zaidi ya shilingi milioni 70 za Tanzania (milioni 4 za Kenya).

•Msanii huyo wa zamani wa WCB pia alifichua kwamba ameenda katika miji mitano kwa ajili ya kurekodi video hiyo.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Staa wa Bongo Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny amefichua kwamba ametumia wiki nzima kurekodi video yake ya muziki ijayo.

Katika taarifa yake ya Jumatano, bosi huyo wa lebo ya Next Level Music aliweka wazi kwamba shughuli ya kurekodi video yake ijayo imemgharimu zaidi ya shilingi milioni 70 za Tanzania (milioni 4 za Kenya).

Rayvanny alisema kwamba alichukua hatua hiyo kubwa ili kuwapa mashabiki wake muziki na video zenye ubora.

"Nimetumia siku saba kushoot video yangu ijayo na kila siku sio chini ya 10M kushoot," alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Aliongeza, "Yote ni kuhusu muziki mzuri na video nzuri kwa mashabiki wangu,"

Msanii huyo wa zamani wa WCB pia alifichua kwamba ameenda katika miji mitano kwa ajili ya kurekodi video hiyo.

Hata hivyo, mwanamuziki huyo hakufichua video hiyo ni ya wimbo wake upi wala wakati ambao anapanga kuiachia.

Takriban miezi miwili iliyopita, Rayvanny aliweka wazi jinsi alivyoratibu bajeti ya kufanya video ya ngoma yake Nitongoze akimshirikisha Diamond Platnumz.

Mwimbaji huyo wa Bongo alipakia mazungumzo kwenye mtandao wa Instagram akielezea jinsi walishirikiana na muelekezaji wake Ivan kufanikisha video hiyo ambayo ilitajwa kugharimu kiasi kikubwa cha pesa.

Alisema kuwa alitoa ombi kwa  Ivan kwamba alikuwa anahitaji watu zaidi ya mia mbili kushirikishwa, huku wote wakiwa katika suti maalum kwa ajili ya video hiyo – kama ilivyoonekana kwenye video yenyewe.

Ivan alimwambia kuwa watu hao 200 kupatikana si tatizo lakini akamwambia kizingiti kikubwa kilichokuwa mbele yake ni kwamba kila mmoja alikuwa anataka kuvaa suti ya thamani ya laki 2 pesa za Tanzania ili kushiriki katika video hiyo.

Kwa mshangao mkubwa kwa Ivan, Rayvanny alikubali kwa haraka kuwa angegharamia suti zote mradi tu video iwe ya haiba iliyotukuka.

Kwa hesabu za haraka, suti 200 kila moja ikigharimu laki mbili ni sawa na shilingi milioni 40 pesa za Tanzania. Takrima hiyo ukiibadilisha katika hela za benki kuu ya Kenya zinakuja zaidi ya milioni mbili.

Hapo awali, Diamond ambaye alishirikishwa kwenye wimbo huo alimsifia kwa njia ya kipekee Rayvanny kwa kutokuwa bahili katika kumwaga pesa ili kufanikisha video ambayo aliitaja kama ya kimataifa.

“#Nitongoze Video ya Rayvanny akimshirikisha Simba ishatoka sasa…Kaitizame kwenye bio ya @rayvanny … Hela umewekeza kwenye Video Chui, Ninajihisi fahari kuwa katika mradi huu wako kaka,” Diamond alisema.