Tanasha Donna adokeza kuhusu kuchumbiwa baada ya kuondoka nyumbani kwa Diamond

Tanasha amedokeza kwamba ameombwa ndoa na mwanaume ambaye hajafichua.

Muhtasari

•Mpenzi huyo wa zamani wa  Diamond alidokeza kwamba huenda akakubali kuolewa na mtu huyo ambaye hajajulikana.

•Mapema mwezi huu, Tanasha alionekana kwenye jumba la kifahari la  Diamond Platnumz jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Image: INSTAGRAM// TANASHA DONNA

Mwimbaji wa Kenya Tanasha Donna amedokeza kwamba ameombwa ndoa na mwanaume ambaye hajafichua.

Katika chapisho lake la hivi punde kwenye mtandao wa Instagram, mpenzi huyo wa zamani wa staa wa bongo Diamond Platnumz alidokeza kwamba huenda akakubali kuolewa na mtu huyo ambaye hajajulikana.

Tanasha Donna hata hivyo alimtaka mtu huyo amsubiri kwanza amalize kutia saini kwenye mkataba wa mamilioni.

"Naweza kusema NDIYO kubwa kwako, lakini ngoja kwanza nisaini mkataba huu wa dola milioni 1.5 Inshallah," alisema.

Mama huyo wa mvulana mmoja wa miaka minne hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu taarifa  hiyo yake.

Mapema mwezi huu, Tanasha alionekana kwenye jumba la kifahari la mzazi mwenzake Diamond Platnumz jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Katika video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, mwanamuziki huyo alionekana akiwa amepumzika kwenye kochi nyumbani kwa Diamond pamoja na mwanawe Naseeb Junior. Hiyo Ilikuwa ni safari ya kwanza kwa Bi Donna kwenda nyumbani kwa staa huyo wa Bongo takriban miaka mitatu baada ya kutengana kwao.

Tanasha pia aliweza kuungana na familia ya Diamond baada ya miaka mingi bila kuona.

Katika msururu wa video zilizochapishwa na Diamond, bosi huyo wa WCB angeweza kuonekana akibadilisha nepi ya mtoto wake.

Baadaye, wawili hao walishiriki wakati mzuri wa baba namwana ambapo Diamond alisikika akimfundisha mtoto huyo wake wa miaka minne jinsi ya kusoma na kutambua wanyama tofauti tofauti na sauti zao.

Diamond na Tanasha walitengana mwaka wa 2020 baada ya kumkaribisha mtoto wao Naseeb Junior. Tangu wakati huo, wamekuwa wakishirikiana katika malezi huku wakiwasiliana na mara kwa mara kuhusu suala hilo.

Akizungumza kwenye mahojiano na Mpasho mwaka jana, Tanasha aliweka wazi kuwa hakuwa kwenye mahusiano yoyote wakati huo.

Mzazi mwenza huyo wa Diamond pia alidokeza kwamba alikuwa tayari kumpa mwanaume mwingine nafasi katika moyo wake.

"Nipo single! Labda kuna mtu ambaye anaweza kuwa mpenzi anayefuata, inaweza kuwa," alisema mwezi Julai.

Mama huyo wa mvulana mmoja alibainisha kuwa hazingatii  sura ya mwanaume wala utajiri wake anapotafuta mchumba.

Alifichua kuwa jambo la msingi analozingatia kwa mwanamume  anayekusudia kuchumbiana naye ni tabia yake.

"Tabia ni muhimu sana kwangu. Ni ufunguo wa kila kitu maishani kwa sasa kando na Mungu, mimi ni muumini pia," Alisema.

Tanasha pia alidokeza kuwa mwanaume anayetazamia kuchumbiana naye ni sharti awe mwenye bidii na Mcha Mungu.

"Lazima awe na bidii, lazima awe muumini. Mtu ambaye anaweka Mungu mbele, ni lazima umpende Mungu zaidi ya unavyonipenda. Ni lazima uwe unafanya kitu kwa sababu pia mimi najaribu kujifanyia kitu. Kama hutengenezi kitu kwa ajili yako nitaona kama wewe ni mzembe ama huweki bidii ya kutosha. Sio lazima uwe tajiri lakini lazima uwe unafanya kazi kwa bidii," Alisema Tanasha.

Pia alisema ni sharti mwanaume ambaye anamdai awe na maono kadhaa anayolenga kutimiza maishani.