"Asante baba!" Nillan ajawa bashasha baada ya babake, Diamond kumnunulia zawadi ghali

Diamond amemnunulia mwanawe Prince Nillan zawadi ya simu mpya kabisa ya iPhone 14 Pro Max.

Muhtasari

•Zari alipokea zawadi hiyo aliyotumwa na mzazi mwenzake na kumkabidhi mtoto wao nyumbani kwao Afrika Kusini.

•Haya yanajiri takriban mwezi mmoja tu baada ya Diamond kumzawadi binti yake Tiffah Dangote kwa simu kama hiyo.

Image: INSTAGRAM// PRINCE NILLAN

Staa wa Bongo, Diamond Platnumz amemnunulia mwanawe Prince Nillan zawadi ya simu mpya kabisa ya iPhone 14 Pro Max.

Prince Nillan, ambaye ni mtoto wa pili wa Diamond na mwanasosholaiti wa Uganda, Zari Hassan alijawa na furaha baada ya kupokea zawadi hiyo ghali. iPhone 14 Pro Max kwa sasa inauzwa kwa takriban shilingi laki mbili nchini Kenya.

Zari alipokea zawadi hiyo aliyotumwa na mzazi mwenzake na kumkabidhi mtoto wao nyumbani kwao Afrika Kusini.

"Na sasa. Je, utasema asante kwa baba?" alimuuliza mwanawe.

Prince Nillan ambaye alishikilia simu hiyo yake mpya kwa nguvu baada ya kukabidhiwa na kuonekana kushindwa kabisa kuficha hisia ya furaha alisema, "Asante baba!" na kuendelea kuonyesha tabasamu kubwa tu.

Mama yake, Zari baadaye alichukua iPad ambayo amekuwa akitumia kwani hakuihitaji tena kuona sasa amepata simu.

Haya yanajiri takriban mwezi mmoja tu baada ya bosi huyo wa WCB kumzawadi binti yake na Zari, Tiffah Dangote kwa simu kama hiyo hiyo ya iPhone 14 Pro Max ambayo ndiyo mbichi zaidi kwenye soko ya iPhone.

Zawadi hiyo ilipokelewa kwa shangwe na shukrani na Tiffah, ambaye alionyesha video kwenye TikTok akifungua zawadi hiyo.

Kwenye video hiyo, Tiffah alisikika akimshukuru baba yake kwa zawadi hiyo huku mama yake, Zari Hassan akirekodi tukio hilo.

Diamond anajulikana kuwathamini wanawe na watu wanaohusiana naye na mara kwa mara ameonekana akiwazawadia zawadi za bei ghali.

Takriban wiki mbili zilizopita, staa huyo wa Bongo alishiriki muda mzuri na mwanawe mdogo, Naseeb Junior. Diamond alionekana hadharani na mtoto huyo wake na Tanasha Donna kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu walipohudhuria hafla ya kumtambulisha mtoto wa mwanaspoti Haji Manara.

Baadaye, baba huyo wa watoto wanne wanaojulikana alichapisha picha zake na mwanawe wakiwa ndani ya gari lake la kifahari aina ya Rolls Royce. Wawili hao walivalia kanzu nyeusi zinazofanana na walionekana kuwa na muungano mzuri.

"@naseeb.junior❤️🌹," aliandika chini ya picha hizo ambazo alipakia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Picha zingine zilimuonyesha akiwa amemshika mvulana huyo wa miaka mitatu.