Mama Dangote ajawa bashasha baada ya Zuchu kumuonyesha upendo licha ya kumtema mwanawe, Diamond

Mamake Diamond alimshukuru Zuchu kwa zawadi hiyo maalum na kuonyesha kuwa ameipenda.

Muhtasari

•Mama Dangote alionyesha video yake akiwa amevalia dera ambalo alifichua kwamba lilikuwa ni zawadi kutoka kwa Zuchu.

•Hatua ya  Zuchu inaonyesha kuwa amedumisha uhusiano mzuri na familia ya Diamond licha ya yaliyotokea

Diamond, Mama Dangote, Zuchu
Image: HISANI

Mamake Diamond Platnumz, Bi Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote alijawa na bashasha baada ya aliyetarajiwa kuwa mkwe wake, Zuchu kumzawadia dera zuri.

Siku ya Ijumaa, mzazi huyo wa bosi wa WCB alionyesha video yake akiwa amevalia dera ambalo alifichua kwamba lilikuwa ni zawadi kutoka kwa Zuchu.

Kwenye video hiyo, Mama Dangote alimshukuru msanii huyo wa mwanaye kwa zawadi maalum na kuonyesha wazi kuwa ameipenda.

"Asante @officialuchu kwa dera zuri!" aliandika.

Dera hilo linaonekana kuwa zawadi maalum ya Zuchu kwa mamake Diamond wakati yeye na waislamu wengine wakiadhimisha mwezi mtukufu wa Ranadhan.

Haya yanajiri takriban mwezi mmoja tu baada ya binti huyo mdogo wa gwiji wa taarab wa Zanzibar, Khadija Kopa na Diamond kutangaza kuvunjika kwa mahusiano yaliyoaminika kuendelea kwa muda mrefu.

Mwezi Februari, Zuchu aliibua wasiwasi juu ya hali ya mahusiano yake kufuatia chapisho lake kwenye mtandao wa Snapchat.

Mwimbaji huyo wa kibao 'sukari' alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.

"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'

Mwimbaji huyo kutoka Zanzibar pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond kwenye mtandao wa Instagram.

Baadaye, Diamond alizamia kwenye mtandao wa Instagram kuthibitisha kutengana na msanii huyo wake katika WCB.

Katika taarifa yake, bosi huyo wa WCB aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena. Alibainisha kuwa yeye na malkia huyo wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa  kati yao.

"Kwa pamoja na Zuhura tunaomba tuwataarifu ya kwamba, kwa sasa sisi ni dada na kaka na si wapenzi kama ilivyokuwa ikidhaniwa ama wengine kujua.. Mnaruhusiwa wachumba na wake ama waume kama tutawaridhia," alisema.

Diamond aliongeza, "Lakini muwe na vibarua vinavyoeleweka  sio mje kutuchuna, maana atuhongi hovyo."

Baadae hata hivyo, alionyesha mahaba makubwa kwa msanii  huyo wake kwa kumnunulia pambo la bei ghali.

Diamond akiwa jijini London, Uingereza alionekana kwenye video akiwa ameshika cheni maridadi ya fedha yenye kichwa cha malkia ambayo alinunua katika duka moja la mapambo jijini humo.

Kulingana na taarifa kwenye ukurasa rasmi wa Wasafi, alinunua cheni hiyo inayomeremeta maalum kwa Zuchu.

"Simba amenunulia Zuchu pambo jipya kabisa jijini London," taarifa hiyo ilisoma.

Wimbo wao 'Mtasubiri' ambao unawasuta wanaochukia uhusiano wao uliambatanishwa na video hiyo.

Hatua ya hivi punde ya Zuchu inaonyesha kuwa amedumisha uhusiano mzuri na familia ya Diamond licha ya yaliyotokea.