Baba wa kambo wa Diamond afunguka kuzaa mtoto na Mama Dangote

Shamte alisisitiza kwamba ameridhika sana na Mama Dangote kuwa mwenzi wake wa maisha

Muhtasari

•Shamte aliweka wazi kuwa mke wake bado ana umuhimu mkubwa kwake licha ya kutopata mtoto yeyote naye.

•Shamte aliweka wazi kuwa anawapenda na kuwakubali watoto wote ambao wametambuliwa kuwa wanawe Diamond.

Uncle Shamte, Diamond Platnumz na Mama Dangote
Image: HISANI

Mfanyibiashara Uncle Shamte amepuuza shinikizo la jamii kumtaka apate mtoto na mkewe Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote.

Katika mahojiano na Mbengo TV, baba huyo wa kambo wa staa wa Bongo Diamond Platnumz, aliweka wazi kuwa mke wake bado ana umuhimu mkubwa kwake licha ya kutopata mtoto yeyote naye.

Bw Shamte alisisitiza kwamba ameridhika sana na Mama Dangote kuwa mwenzi wake wa maisha.

"Mimi naona faida yake yeye (Mama Dangote) ata kama hakunizalia mtoto. Kuwa mke wangu tu ni faida. Namheshimu, Nampenda. Iko hivyo," alisema.

Wakati huo huo, mfanyibiashara huyo alizika tetesi kuwa mahusiano yake na Mamake Diamond yamefika kikomo. Madai kuwa wametengana yaliibuka baada ya kubainika kuwa hawafuatiliani tena kwenye mtandao wa Instagram.

Alibainisha kuwa kupungua kwa shughuli za mitandao ya kijamii kati yao ni jambo la kawaida na haimaanishi wametengana.

"Ni masuala ya kawaida. Yule ni binadamu na mimi ni binadamu. Mbona muda mrefu yeye hanipost na mimi simpost. Ni kawaida," alisema.

Pia aliweka wazi kuwa anawapenda na kuwakubali watoto wote ambao wametambuliwa kuwa wanawe Diamond.

"Mama Naseeb anawakubali wote. Naseeb anaakubali watoto wake wote. Mimi ni nani?" alisema.

Shamte ni miongoni mwa watu wengi waliovutiwa na picha nzuri za Diamond na mtoto wake mdogo, Naseeb Junior.

Shamte ambaye amekuwa akichumbiana na mamake Diamond, Mama Dangote, kwa muda mrefu aliwasherehekea wawili hao kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatatu na kuonyesha upendo kwao.

Kwenye Instastori zake, alichapisha video na picha za Diamond na mwanawe na chini yake  kuweka na  emoji za moyo.

"@DIAMONDPLATNUMZ & NASEEB.JUNIOR ❤❤," aliandika.

Pia alichapisha picha zingine nzuri za wawili hao na chini yake akaweka emoji mbili za nyuso za simba.

Mama Dangote pia alimsherehekea mwanawe pamoja na mjukuu huyo wake. Alichapisha picha za wawili hao na kuwataja kuwa mapacha.

"Pachaaaaaa @diamondplatnumz @naseeb.junior 🧡🧡," aliandika