“Nitakupeleka polisi!” TID atema cheche kwa wasanii wa Arbantone kutumia nyimbo zake

'Ukichukua wimbo wangu unapeleka na kufanya hiyo Arbantone yako bila ruhusa yangu utakuwa umejiingiza matatani ndugu yangu na nitakuchukia katika maisha yangu yote,” TID alisema.

Muhtasari

• Aghalabu, wasanii hao huchukua tu kazi hizo haswa za kizamani bila hata ridhaa kutoka kwa mmiliki wa muziki asili.

• Akiulizwa kuhusu hilo wakati alipotimba katika klabu ya starehe ya Quiver Jumatano, TID alisema kwamba haruhusu hilo kufanyika kwa kazi zake za Sanaa bila ridhaa yake.

 

TID
TID
Image: INSTAGRAM

Msanii mkongwe kutoka Tanzania, Top In Dar maarufu kama TID Mnyama ametoa onyo kali kwa wasanii wa aina mpya ya muziki wa Kenya, Arbantone dhidi ya kufanya masihara kwa kutumia baadhi ya muziki wake kwenye ngoma zao.

Muziki wa Arbantone ni aina mpya ambayo msanii anachukua ngoma za wasanii na mitindo tofauti tofauti kisha anazichanganya na kuifanya kuwa ngoma moja.

Aghalabu, wasanii hao huchukua tu kazi hizo haswa za kizamani bila hata ridhaa kutoka kwa mmiliki wa muziki asili.

Akiulizwa kuhusu hilo wakati alipotimba katika klabu ya starehe ya Quiver Jumatano, TID alisema kwamba haruhusu hilo kufanyika kwa kazi zake za Sanaa bila ridhaa yake.

TID alisema kwamba iwapo msanii wa Arbantone angependa kutumia baadhi ya nyimbo zake, basi sharti mwanzo awasiliane naye la sivyo atampeleka polisi na kisha kumchukia maisha yake yote.

“Aisee nitakufunga polisi, usifanye hicho kitu. Ukichukua wimbo wangu unapeleka na kufanya hiyo Arbantone yako bila ruhusa yangu utakuwa umejiingiza matatani ndugu yangu na nitakuchukia katika maisha yangu yote,” TID alisema.

Kuhusu kukimya kwa muda mrefu kutoka kwenye jukwaa la Sanaa ya muziki, TID alisema kwamba kando na muziki, yeye pia ni muigizaji na ameshiriki katika filamu za tamthilia nyingi tu huku pia akizungumzia vitu anavyotarajia kuvifanya siku zijazo.

“Kuna tamthilia ambazo nimefanya nafikiri bado hawajazindua lakini pia niko na shoo zangu kwenye runinga zinakuja, niko na podikasti yangu na mambo mengine mengi yanakuja kwa hiyo watu wakae kufikiria nini kitakuja mwanzo, tukiwaambia mambo mengi tunawachanganya,” alisema.