Harmonize azidisha mzozo wake na Diamond, aelekea mahakamani

Konde Boy ametafuta mawakili kumsaidia kushtaki WCB kwa kunufaika na jasho lake.

Muhtasari

•Harmonize ametafuta huduma za mawakili kumsaidia kuishtaki WCB kwa madai ya kunufaika na jasho lake.

•Harmonize anadai kuwa mirabaha yake inaenda kwenye akaunti ya WCB badala ya yake licha ya mkataba wake kusitishwa.

katika siku za urafiki wao.
Harmonize na Diamond katika siku za urafiki wao.
Image: HISANI

Ugomvi mkubwa wa mastaa wawili wa bongo, Harmonize na Diamond Platnumz unaonekana kuwa tayari kuongezeka huku mwanzilishi huyo wa Kondegang sasa akitishia kumshtaki bosi huyo wake wa zamani.

Harmonize almaarufu Konde Boy, ambaye aliondoka Wasafi mwaka wa 2019 ametafuta huduma za mawakili kumsaidia kuishtaki lebo hiyo inayomilikiwa na  Diamond kwa madai ya kunufaika na jasho lake.

Mwimbaji huyo anasema WCB imeshirikiana na wasambazaji wa muziki, Mziiki, kuchukua fedha zinazotokana na muziki wake akidai kuwa zinaenda kwenye akaunti ya lebo hiyo badala ya yake licha ya mkataba wake kusitishwa.

“Wasafi na Mziiki wameshirikiana kunichafua ila sijawakosea. Imekuwa kibarua kubwa kupata kile ambacho ni changu kutoka kwao ili niweze kulisha familia yangu kama wanavyofanya na familia zao," alisema.

"Kwa nini waninyime kupata haki yangu ya Haki Miliki (IP) huku wakiendelea kukusanya pesa kutoka kwa IPs zangu kwa niaba yangu,” alihoji.

Mwimbaji huyo wa 'Single Again' alisema anakamilisha mipango na mawakili wake ili kupeleka kesi hiyo mahakamani hivi karibuni.

Pia ametoa wito kwa Waziri Msaidizi mpya wa Utamaduni na Sanaa, rapa Mwana FA, kumsaidia kutatua mzozo huo.

"Ninamtegemea atanisaidia kwa sababu nimeshindwa kukusanya mirabaha yangu ya muziki kwa miaka mitatu,” alisema.

Mwezi uliopita, Harmonize aliweka wazi kuwa anahitaji mirabaha yake ya miaka mitatu ambayo WCB imekuwa ikienda kwa WCB.

"Wasafi na Mziiki wameshirikiana kuchezea maisha yangu, na sikuwafanyia chochote ubaya unaanza pale mtu unapotaka jasho lako ili uisaidie familia yako kama ao wanavyofanya.

Unaweza aje kukaa na haki ya mtu wakati anaipambania miaka mitatu unachukua wewe huogopi hata laana ya Mungu," alisema.

Mwimbaji huyo alisema yuko tayari kufa akipigania haki zake pamoja na wasanii wenzake mradi awe ameacha utajiri mkubwa kwa binti yake.