Fathermoh afichua kwa nini alikataa ombi la babake kutaka aimbe injili na kuacha Gengetone

"Kwa sababu mimi nafikiri watu wengi Kenya wamejitenga na injili, sasa unaona wengi wanaondoka huo mrengo. Ningependa sana lakini sasa ona kina Willy Paul, Bahati walitoroka huko, kumaanisha kuna kitu." alisema.

Muhtasari

• Baada ya babake kugundua kwamba anaimba muziki huo kupitia kwa mjomba wake, alimfuata na kumuuliza kwa nini hakutaka ajue kuwa anaimba.

FATHERMOH
FATHERMOH
Image: Facebook

Msanii wa gengetone, Fathermoh kwa mara ya kwanza amefichua jinsi baba yake aligundua kuwa anaimba muziki wa aina hiyo na ushauri aliompa.

Akizungumza kwenye mahojiano katika kituo kimoja cha redio humu nchini, Fathermoh alisema kwamba katika maisha yake tangu ajiunga na kidato cha kwanza, amekuwaakilelewa na baba baada ya mamake kuaga dunia.

Mkali huyo wa ‘Kaskie vibaya’ alisema kwamba baada ya kumaliza kidato cha nne, alijiajiri katika biashara ya kuuza kanda mbili lakini wakati huo huo pia akaanza kufanya muziki wa Gengetone.

Hata hivyo, hakuweza kumambia babake kutokana na kasumba ambayo ilikuwa imetawala kwamba Gengetone ni muziki wenye maudhui chafu.

Baada ya babake kugundua kwamba anaimba muziki huo kupitia kwa mjomba wake, alimfuata na kumuuliza kwa nini hakutaka ajue kuwa anaimba.

“Baba alinifuata na kuniuliza ni lini ningemwambia kuwa naimba, aliniambia kuwa alikuwa ametaarifiwa mwezi mmoja kabla ya kuniuliza lakini alikuwa anasubiria nimwambie. Lakini hakukasirika, aliniambia kama inaleta pesa niendelee, juu yeye huwa hasikilizi hizo nyimbo,” Fathermoh alisema.

Hata hivyo, msanii huyo alifichua kwamba babake kwa wakati mmoja alimfuata na kumshauri kujaribu kutunga nyimbo za injili lakini alikataa akisema kuwa huenda mapato yake ya kifedha yakadorora ikiwa atafuata ushauri huo wa babake.

“Babangu huniambia yeye hasikilizi hizo nyimbo, kwa hiyo hajali, yeye ako tu. Lakini kuna wakati mmoja aliwahi niambia ‘unaweza jaribu injili’. Nikamwambia hata mimi naweza penda kufanya injili lakini tutalala njaa.”

“Kwa sababu mimi nafikiri watu wengi Kenya wamejitenga na injili, sasa unaona wengi wanaondoka huo mrengo. Ningependa sana lakini sasa ona kina Willy Paul, Bahati walitoroka huko, kumaanisha kuna kitu. Lakini uhusiano wangu mimi na Mungu ni ule wa karibu sana, huwa naomba asubuhi na usiku kila wakati,” Fathermoh alifafanua.