Maajabu! Harmonize na mzazi mwenzake Diamond, Zari Hassan waonyeshana upendo mkubwa

Harmonize amekuwa akijivunia maisha ya ukapera baada ya kutengana na Kajala Masanja mwaka jana.

Muhtasari

•Zari alitengeneza video ya kuburudisha kwenye mtandao wa Tiktok na kutumia wimbo wa Harmonize 'Single Again.'

•Harmonize alikiri heshima yake kubwa kwa mfanyibiashara huyo ambaye kwa sasa anaishi Afrika Kusini.

wameonyeshana upendo mkubwa kwenye Instagram
Harmonize na Zari Hassan wameonyeshana upendo mkubwa kwenye Instagram
Image: HISANI

Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize na mwanasosholaiti wa Uganda, Zari Hassan wamewaacha mashabiki wao vinywa wazi baada ya kuonyeshana upendo mkubwa na kuthaminiana.

Zari Hassan ambaye ni mpenzi wa zamani wa hasidi mkubwa wa Harmonize, Diamond Platnumz alitengeneza video ya kuburudisha kwenye mtandao wa Tiktok na kutumia wimbo wa bosi huyo wa Konde Music Worldwide 'Single Again.'

"Huyo Shangazi mmoja tajiri ambaye huwa anajigamba jinsi alivyoolewa na bilionea. Sasa amepewa talaka na prenup.. Kurudi kwenye nyumba ya familia,"  mwanasoshalaiti huyo aliandika kwenye video hiyo ambayo ilimuonyesha kama kwamba anarudi nyumbani kwao akiwa amevunjika moyo.

Harmonize alionekana wazi kufurahishwa na kitendo cha mama huyo wa watoto watano na hata akachapisha video hiyo kwenye ukurasa wake wa Instragram.

Wakati huo, mwimbaji huyo wa bongo alikiri heshima yake kubwa kwa mfanyibiashara huyo ambaye kwa sasa anaishi Afrika Kusini.

"Nimeipost mara mbili kwa sababu ni boss lady. Heshima kubwa kwa bosi @zarithebosslady," Konde Boy  aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo ambayo kwa kawaida hutumika kuashiria upendo kwa mtu.

Kitendo hicho kinaonekana kuwa chenye utata ikizingatiwa kwamba Zari ni mzazi mwenza wa mpinzani mkuu wa Harmonize kwenye tasnia ya Bongo, Diamond Platnumz. Ingependeza kuona jinsi Diamond amekipokea.

Zari na Diamond wamedumisha uhusiano mzuri na wameendelea kushirikiana katika malezi licha ya kutengana takriban miaka mitano iliyopita. Video iliyowaonyesha wakidensi pamoja ilivuma mitandaonI hivi majuzi.

Mwaka jana, mwanasosholaiti huyo aliweka wazi kuwa anashirikiana vizuri na  Diamond katika malezi ya watoto wao wawili.

Katika mahojiano na Wasafi Media, Zari alifichua kuwa yeye na staa huyo wa Bongo wamekuwa wakijadiliana mara kwa mara kuhusu njia bora ya kuwalea watoto wao, Tiffah Dangote na Prince Nillan.

"Tumefanya malezi ya kushirikiana kuwa rahisi sana. Tumekuja pamoja na kusema tunataka bora zaidi kwa watoto wetu,tunaketi na kuongea," Zari alisema.

"Tuna maslahi yao bora moyoni; wanataka nini? wanataka kuenda wapi? wanajiona wapi?"

Mama huyo wa watoto watano alibainisha kuwa kuelewana kwake na Diamond kumerahisisha ushirikiano wao katika malezi.

Harmonize kwa upande wake amekuwa akijivunia maisha ya ukapera baada ya kutengana na muigizaji Frida Kajala Masanja mwishoni mwa mwaka jana. Wawili hao waliachana baada ya kuwa pamoja kwa miezi kadhaa.