Wanawe Zari wazidiwa na hisia baada ya kutembelea kaburi la baba yao Ivan Ssemwanga

Pinto, Raphael na Quincy walitembelea kaburi la marehemu Ivan Ssemwanga nchini Uganda.

Muhtasari

•Watatu hao walionekana wenye huzuni na mawazo tele huku wakirandaranda karibu na  kaburi la baba yao.

•Haya yanajiri takriban miezi miwili tu baada ya Zari Hassan kutembelea kaburi hilo la aliyekuwa mumewe.

Zari na wanawe
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Wana watatu wa kwanza wa mwanasosholaiti mashuhuri Zari Hassan walitembelea kaburi la marehemu baba yao, Ivan Ssemwanga katika kijiji cha Nakaliro, katika Mji wa Kayunga, nchini Uganda.  

Siku ya Jumatano, mama huyo wa watoto watano alichapisha video ya wanawe, Pinto Ttale, Raphael Ssemwanga na Quincy Ssemwanga wakiwa wamesimama katika eneo la makaburi ambapo Bw Ssemwanga alizikwa.

Watatu hao walionekana wenye huzuni na mawazo tele huku wakirandaranda karibu na  kaburi la baba yao.

“Iko vizuri wanangu🙏” Zari aliwafariji wanawe.

Haya yanajiri takriban miezi miwili tu baada ya mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz kutembelea kaburi hilo la aliyekuwa mumewe.

Zari aliandamana na watu wengine kadhaa akiwemo mpenziwe wa sasa Shakib Cham Lutaaya wakati alipotembelea kaburi hilo lililo mwezi Januari. Alirekodi video fupi ikimuonyesha akiwa amekaa kwenye kaburi hilo la baba wa watoto wake watatu wa kwanza huku watu wengine ambao walikuwa wameandamana naye wakipumzika kuzunguka eneo hilo.

Mfanyibiashara huyo ambaye kwa sasa anaishi Afrika Kusini amekuwa akitembelea kaburi la Ivan mara kwa mara tangu mume huyo wake wa zamani alipoaga dunia mnamo Mei 25, 2017 baada ya kuugua.

Bw Ssemwanga, ambaye alikuwa mfanyibiashara tajika nchini Afrika Kusini alifariki katika hospitali ya Steve Biko Academic, jijini Pretoria, Afrika Kusini ambako alikuwa amekimbizwa akiwa katika hali mbaya.

Baadaye alizikwa kijijini kwao Nakaliro katika hafla ghali iliyohudhuriwa na watu maarufu na matajiri nchini Uganda na kwingineko ikiwa ni pamoja na wanamuziki Jose Chameleone, Bobi Wine, SK Mbuga na Weasel.

Kiasi kikubwa cha pesa na mvinyo ghali vilimwagwa ndani ya kaburi la mfanyibiashara huyo baada ya jeneza lake kuteremshwa. 

Ssemwanga ambaye alitambulika kama kiongozi wa Rich Gang nchini Uganda alifariki akiwa na umri wa miaka 39 na aliacha nyuma watoto watatu wa kiume ambao alikuwa amepata na mwanasoshalaiti Zari Hassan.

Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya mwongo mmoja na kujaliwa watoto watatu pamoja kabla ya kutengana. Baadae Zari alijitosa kwenye mahusiano na Diamond na kupata watoto wengine wawili naye.