Boni Khalwale afurahi baada ya mbuzi aliyekataa kuchinja Krismasi kuzaa mapacha

Seneta huyo alisema kuwa mbuzi huyo alikuwa ni zawadi ya Krismasi ambayo binti wake alimpa kama kitoweo lakini akakataa kumchinja na kuamua kumfuga.

Muhtasari

• Khalwale anafahamika na Wakenya wengi kwa jinsi anavyoisherehekea familia yake katika matukio madogo madogo.

Boni Khalwale afurahia mbuzi wake kupata mapacha
Boni Khalwale afurahia mbuzi wake kupata mapacha
Image: Twitter

Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale ni mtu mwenye furaha baada ya mbuzi wake kuzaa mapacha.

Khalwale ambaye hakawii kushiriki matukio ya familia yake kwenye mtandao wake wa Twitter alipakia picha ya mbuzi huyo akiwanyonyesha watoto wake mapacha.

Seneta huyo alifichua kwamba mbuzi huyo ni zawadi ambayo alipewa na binti wake mwaka jana msimu wa Krismasi kama kitoweo lakini alikataa kumchinja na badala yake kuamua kumfuga.

“Ni mambo madogo madogo ambayo hufanya maisha yangu. Binti yangu, Inger Imbuhila alinipa zawadi ya Krismasi, ambayo nilikataa kuchinja. Sasa angalia amefanya nini! Mapacha!” Khalwale alisema.

Khalwale anafahamika na Wakenya wengi kwa jinsi anavyoisherehekea familia yake katika matukio madogo ikiwemo kuzaliwa kwa mtoto, kufuzu katika mitihani ya kitaifa miongoni mwa mengine.

Miezi kumi iliyopita, Khalwale alifurahi mtoto alipozaliwa kwenye boma lake na kupitia Twitter aliandika ujumbe mzuri akisema kuwa mtoto huyo aliyezaliwa alikuwa anamkumbusha na pia kuziba pengo la marehemu mke wake wa kwanza aliyefariki.

“Baraka kwa wingi. Jana usiku katika Hospitali ya Nairobi, kusubiri kwa muda mrefu kuzaliwa upya kwa mke wangu marehemu Adelaide Shikanga Khalwale kulifikia mwisho wa furaha. Mungu aliibariki familia yangu na CANDICE SHIKANGA KHALWALE. Hongera sana @TKhalwale kwa ajili ya kuziba pengo lililoachwa na kifo cha mama yako,” aliandika Khalwale kwa furaha.

Mheshimiwa Khalwale amekuwa akigonga vichwa vya habari kila mwaka haswa matokeo ya mitihani ya kitaifa yanapotangazwa na Waziri wa elimu kutokana na dhana kwamba yeye kwa miaka ya hivi karibuni amekuwa akisherehekea mmoja kati ya wanafamilia wake kufuzu katika mitihani hiyo.