Alex Mwakideu ajiuzulu kutoka Milele FM baada ya miaka 5

Mwakideu alidokeza kwamba hatakuwa nje kwa muda mrefu kwani kuna mahali anaelekea baada ya kuondoka hewani.

Muhtasari

•Mtangazaji huyo ambaye amekuwa katika kituo hicho kwa miaka 5 aliwashukuru mashabiki wake kwa kumpa masikio yao wakati alipokuwa hewani.

•Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah kujiuzulu kutoka katika kituo hicho.

Image: FACEBOOK// ALEX MWAKIDEU

Mwanahabari maarufu mzaliwa wa Pwani, Alex Mwakideu amegura kituo cha Media Max Ltd, Milele FM.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, mtangazaji huyo ambaye amekuwa katika kituo hicho cha redio kwa takriban nusu muongo aliwashukuru mashabiki wake kwa kumpa masikio yao wakati alipokuwa hewani.

“Yoooh!! Imekuwa miaka 5 ndani ya Milele FM. Nimeenjoy!! Acha niseme Ahsante sana kwako msikilizaji, kwa sababu bila wewe hakuna redio! Wewe ndio unatufanya tufanye hivi inaitwa Radio,” Mwakideu alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Pia alichukua fursa hiyo kuwashukuru waliokuwa wenzake na kuashiria kwamba walijitolea kwa kila kitu. Wakati huo huo, alidokeza kwamba hatakuwa nje kwa muda mrefu kwani kuna mahali anaelekea baada ya kuondoka Milele.

“Pia niseme ahsante sana kwa wenzangu wote, hao ninaowaacha, na wale waliotoka Milele FM tayari. Asanteni nyote. Tuliipiga, na Ikapigika!! Ukurasa umefungwa. Kwenda ijayo! Guess tunaenda wapi next,” alisema.

Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah kujiuzulu kutoka katika kituo hicho.

Wakati akitangaza kuondoka kwake Jumanne wiki jana, msanii huyo mwenye umri wa miaka 30 alifichua kuwa aliamua kujiuzulu baada ya yeye na shirika hilo ya utangazaji kutokubaliana kuhusu kandarasi.

""Nimeacha kazi rasmi katika MILELE FM baada ya huduma ya mwaka 1 na miezi 3. Hatukuweza kukubaliana kuhusu baadhi ya vipengele vya kandarasi na mikakati ya kazi hivyo kuisimamisha," Mulamwah alitangaza wiki jana.

Mchekeshaji huyo aliishukuru kampuni ya Media Max kwa kumpa nafasi ya kuwa hewani na pia akawapongeza wafanyakazi wenzake wa zamani kwa kumuonyesha sapoti ndani ya mwaka mmoja na miezi mitatu ambayo amekuwa hapo.

"Kwa mashabiki wa konki asanteni sana , bado tutakutana kwenye majukwaa na vikao vingine vingi. Imekuwa nzuri. nimejifunza mengi - Merci! KONKI,” alisema.

Miongoni mwa watu waliomtakia heri katika mradi wake ujao ni anayedaiwa kuwa mpenzi wake Ruth K.

“kila la kheri mpenzi. Baraka zaidi njiani,” aliandika.