Kukosa heshima? Mercy Tarus afunguka kwa nini aliwazomea vikali Mandago, Bii, Barorot kwenye mkutano

Mercy alieleza jinsi wazazi na wanafunzi walioathirika wanavyoteseka baada ya programu hiyo ya masomo waliyolipia kufeli.

Muhtasari

•Mercy alieleza muktadha wa hali ya kuhuzunisha ambayo waathiriwa wanapitia baada ya kupoteza hela zao, jambo ambalo lilimfanya ajawe uchungu moyoni.

•Pia alifunguka kuhusu hatma ya kusikitisha ya wanafunzi wenzake ambao waliathiriwa vibaya na kufeli kwa programu hiyo ya masomo.

Mercy Tarus ndani ya studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Bi Mercy Tarus, mwanadada jasiri ambaye amekuwa akivuma kwenye mitandao ya kijamii kwa takriban wiki moja baada ya video yake akiwazomea vikali gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii Chelilim, naibu gavana John Barorot na seneta Jackson Mandago kusambaa amefunguka kuhusu  kwa nini alisikika akiwa amejawa na ghadhabu  wakati akiwaongelesha viongozi hao wakuu wa kaunti.

Katika mahojiano ya kipekee na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, mhitimu huyo wa chuo kikuu cha Kabarak alieleza muktadha wa hali ya kuhuzunisha ambayo wazazi na wanafunzi waathiriwa wanapitia baada ya kupoteza hela zao, jambo ambalo lilimfanya ajawe uchungu moyoni.

Mercy alifunguka kuhusu matibabu ghali ya baba yake mgonjwa na ugumu wa maisha ambao familia yake inapitia baada ya kupoteza zaidi ya shilingi milioni moja katika programu hiyo ya masomo ya ng'ambo iliyofeli.

“Ngoja nitoe muktadha, baba yangu anaugua na tunatafuta pesa ya kulipia dawa. Anakunywa dawa mbili kila siku , dawa moja ni shilingi 148 bob, kumaanisha mbili ni mia tatu. Kuna dawa nyingine anakunywa mbili kila siku na moja ni Sh48. Kisha kuna zingine bado,” Mercy alisimulia.

Aidha, alifunguka kuhusu jinsi wazazi wengine walivyojizatiti kuwalipia watoto wao kwenda nchini Canada na Finland ili kutafuta maisha bora kisha hatimaye hela zao zikatoweka kwa njia isiyoeleweka.

“Kuna mwanafunzi ambaye wazazi wake waliuza shamba. Kuna wazazi waliomba mkopo ndio mtoto aende akatafute maisha mazuri. Kuna baba mjane alilipa 4.2milioni kwa wasichana wake watatu. Aliuza eka 5 za shamba. Kuna mwanaume mwingine ako na watoto wawili alilipa Sh3.2 milioni,” alieleza.

Pia alifunguka kuhusu hatma ya kusikitisha ya wanafunzi wenzake ambao waliathiriwa vibaya na kufeli kwa programu hiyo ya masomo.

“Kuna kijana sasa haongei kwa sababu ya msongo wa mawazo. Kuna kijana mwingine haongei vizuri. Kuna mzee wa miaka 75 aliuza shamba ndio watoto wake wakasome,” mhitimu huyo alifunguka.

Mercy alikuwa akijibu madai kuwa alikosa adabu alipokuwa akiwahutubia viongozi wa kaunti ya Uasin Gishu katika mkutano uliofanyika wiki jana.