Mercy Tarus atiririkwa machozi studioni akieleza jinsi alitapeliwa 1m ya babake mgonjwa

"Mimi nililipa pesa zangu 600k mwaka jana na mwaka huu nikalipa 400k… wakati wa mkutano walisema kwamba walitumia busara yao kutumia pesa zetu ili kuwalipia wengine ili kusafiri,”

Muhtasari

• Alisema kwamba licha ya kumaliza chuo mwaka 2021, bado hajapata kazi ya kile alichokisomea lakini bado anazidi kusukuma na maisha.

MERCY TARUS
Image: HISANI

Mercy Tarus ambaye aligonga vichwa vya habari wiki jana baada ya kuonekana kwenye video akiwasuta vikali viongozi wa kauti ya Uasin Gishu ameweka wazi kwa nini alionesha hisia za hasira kwa kiwango kile.

Akizungumza kwenye Radio Jambo na mtangazaji Massawe Japani kwenye kipindi cha Ilikuwaje, Tarus alisema kwamba wazazi wake haswa baba yake ni mgonjwa na anazidi kupambana na ugonjwa lakini alilazimika kukopa kima cha shilingi milioni moja ili kuona binti yake amefanikiwa kwenda Canada.

Tarus alisema kwamba uongozi wa kaunti ya Uasin Gishu uliwataka wazazi kulipa kila mmoja kima alichotajiwa ili watoto wao waende nchi za ughaibuni kujiendeleza kimasomo, kwa Mercy alikuwa aende Canada.

Kwa upande wake Mercy alitoa shilingi laki sita na baadae akaja akatakiwa uongeza laki nne tena kuifanya shilingi milioni moja.

“Baba yangu anaugua ugonjwa ambao seli nyeupe za damu haziwezi kupambana na ugonjwa, anaendelea kuugua na matibabu yake ni ya gharama sana na pia ukizingatia kwamba alikuwa anakaribia kustaafu… na alikopa shilingi milioni ambazo zilienda na maji,” Mercy alisema baina ya machungu.

“Kuna wenye walienda halafu kuna wengine tuko nao hapa… sisi tukaambiwa ikifika Desemba tutakuwa tumeenda, tukalipa pesa kwa haraka kwa sababu ya kuangalia kwamba maisha yanaenda kubadilika,” Tarus alieleza.

“Idadi ya watu ambao hatujasafiri ni 321 na kuna wenye wameenda 278 na mwaka huu wameenda 44. Mimi nililipa pesa zangu 600k mwaka jana na mwaka huu nikalipa 400k… wakati wa mkutano walisema kwamba walitumia busara yao kutumia pesa zetu ili kuwalipia wengine ili kusafiri,” aliongeza, akirejelea mkutano wa wiki jana ambako alionekana akiwasuta viongozi.

Alisema kwamba licha ya kumaliza chuo mwaka 2021, bado hajapata kazi ya kile alichokisomea lakini bado anazidi kusukuma na maisha.

“Mimi ni msusi lakini nyakati za wikendi nauza uji na maandazi. Nilitafuta nab ado natafuta kazi nilisomea lakini sijafanikiwa,” alisema.