Mercy Tarus afichua alivyojipata mtegoni wa programu ya masomo iliyofeli, kiasi cha pesa walizotapeliwa

Walitakiwa kulipa 600,000 ndani ya wiki mbili, kiasi ambacho wazazi wake walichukua mikopo ili kulipia.

Muhtasari

•Mercy alisema kuwa awali walitakiwa kuondoka nchini Kenya ifikapo Desemba mwaka jana lakini hadi sasa bado hawajaenda.

•"Baba yangu hayuko sawa, mama amejaribu kupambana nayo vyema. Baba amekuwa hajisikii vizuri," Mercy alisema.

Mercy Tarus ndani ya studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mercy Tarus, mhitimu wa chuo kikuu ambaye amekuwa akivuma kwa takriban wiki moja baada ya video yake akiwazomea viongozi wa kaunti ya Uasin Gishu kusambaa kwenye mitandao ya kijamii amefunguka kuhusu jinsi alivyojiingiza katika mpango wa masomo ya ng'ambo uliofeli.

Katika mahojiano maalum na Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, Mercy alisema alisikia kuhusu nafasi hizo kutoka kwa rafiki yake aliyeona bango kwenye WhatsApp.

Alisema rafiki yake alimweleza kuwa tayari alikuwa ametuma maombi ya masomo nchini Finland lakini yeye  alichagua kusubiri nafasi za kwenda Canada.

"Waliweka memo ya kuomba nafasi ya kozi. Nilijisalili katika BSIT kufanya diploma katika huduma za kijamii,” Mercy alisema.

Mercy alifichua kwamba waliombwa walipe Ksh 600,000, ambayo kulingana na waandalizi ilikuwa 60% ya jumla ya kiasi kilichohitajika. Walitakiwa kulipa pesa hizo ndani ya wiki mbili,  kiasi ambacho wazazi wake walichukua mikopo ili kulipia.

”Wazazi wangu waliomba mikopo. Baba yangu ni mwalimu, mama pia. Waliomba mikopo na kupata,” alisema.

Mercy aliendelea kufunguka jinsi baba yake amekuwa akiugua na jinsi kupoteza pesa kuliathiri familia yao.

"Baba yangu hayuko sawa, mama amejaribu kupambana nayo vyema. Baba amekuwa hajisikii vizuri. Anaugua Lupus. Anatakiwa kufanyiwa dawa. Ni ghali kabisa,” alisema.

Mercy alisema kuwa awali walitakiwa kuondoka nchini Kenya ifikapo Desemba mwaka jana lakini hadi sasa kuna zaidi ya wanafunzi 300 ambao bado hawajaondoka.