Zuchu akejeliwa huku mamake Diamond akizidi kuonyesha upendo mkubwa kwa Tanasha Donna

Mama Dangote aliamua kutoa shukrani zake kwa Tanasha kwa kumpa zawadi ghali pia.

Muhtasari

•Mamake Diamond na mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna wameendelea kuonyeshana upendo kwa vitendo.

•Mama Dangote alionekana akimsaidia Tanasha kuweka mkufu shingoni huku wanafamilia wengine wakishangilia..

Mama Dangote, Tanasha Donna, Zuchu
Image: HISANI

Mama ya Diamond Platnumz Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote na mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna wameendelea kuonyeshana upendo kwa vitendo.

Siku chache tu baada ya Tanasha kumzawadi Mama Dangote kwa zawadi za gharama kubwa kwa siku yake ya kuzaliwa, nyanya huyo wa mwanawe aliamua kutoa shukrani zake kwa kumpa zawadi ghali pia.

Mwanamuziki huyo ambaye ana mtoto mmoja na Diamond Platnumz alishindwa kuficha furaha yake baada ya mama mkwe huyo wake wa zamani kumpa mkufu wa dhahabu na wa fedha wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa mtoto wake Naseeb Jr ambayo ilifanyika nchini Tanzania mapema wiki hii.

“Asante mama, asante mama!” Tanasha alisikika akimwambia Mama Dangote kwenye video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kwenda kumkumbatia.

Katika video hiyo, mamake Diamond alionekana akimsaidia mama huyo wa mjukuu wake kuweka mkufu shingoni huku wanafamilia wengine waliokuwepo wakishangillia.

Haya yanajiri siku chache baada ya Tanasha kuwasilisha zawadi za siku ya kuzaliwa kwa mama mkwewe huyo wa zamani baada ya kutua Tanzania kwa ajili ya siku ya kuzaliwa ya mtoto wake. Mikufu hiyo imechukuliwa kuwa njia ya Mama Dangote ya kuonyesha shukrani kwa mwimbaji huyo wa Kenya.

Wanamitandao wamebaini uhusiano mzuri kati ya wawili hao na kupongeza kitendo cha Mama Dangote kwa mkwewe huyo wa zamani. Baadhi wameonekana kumkejeli anayedaiwa kuwa mpenzi wa sasa wa Diamond Platnumz, Zuchu wakidokeza kuwa mama wa staa huyo wa bongo anampenda zaidi Tanasha.

Tazama baadhi ya maoni ya wanamitandao;-

@sm_tz10 Tanasha mzuri kuliko wanawake wote na Diamond.

@offcial_jessytz31 Zuchu ata vile viatu vya kimasai vya shanga ajawai pewa maskini.

@aishajoseph33: Mashallah mzuri huyu binti alafu hana mambo mengi.

@nancy.kwambok Zuchu kaenda wapi iyo siku

@unique_spa123 Uzuri dada Zuhura alipewa chupi na bra.

Wiki jana, Mama Dangote alifichua zawadi za bei ghali ambazo Tanasha alimpa hivi majuzi kwa siku yake ya kuzaliwa ambayo ilipita miezi miwili iliyopita. Kifurushi cha zawadi kilijumuisha pesa za Dola ya Marekani na Shilingi ya Tanzania, maua na bidhaa ghali ya urembo.

Kifurushi hicho pia kiliambatanishwa na barua ambapo Tanasha alionekana kumuomba radhi mama mkwe huyo wake wa zamani kwa kuchelewa kwake kumsherehekea.

“Mama, kitu kidogo kwa kutotimiza ahadi yangu. Natumai unaipenda. Heri ya siku ya kuzaliwa mama!! Mwenyezi Mungu akubariki daima. Upendo, T,” ujumbe kutoka kwa Tanasha ulisomeka.

Katika majibu yake, Mama Dangote alionekana kuishiwa kabisa na maneno kutokana na upendo mkubwa alioonyeshwa na mama huyo wa mjukuu wake na kumshukuru tu sana kwa hilo.

“Duuuh natoka zangu site nakutana na Surprise ya zawadi yangu ya birthday kutoka kwa Mama Tom kaka @tanashadonna yani sina cha kusema ila nasema Alhamdullillah,” Mama Dangote aliandika chini ya video ya zawadi za Tanasha ambazo aliziweka kwenye Instagram.