Carrol Sonnie amkejeli ex wake Mulamwah baada ya kudokeza anatarajia mtoto na Ruth K

Carrol Sonnie alitoa maoni ya kikejeli akisema, "Keila sio mtoto wangu wamepata mtoto."

Muhtasari

• Carrol Sonnie alitoa jibu la kejeli kwa habari za aliyekuwa mpenzi wake, Mulamwah kudokeza anatarajia mtoto na rafiki yake mkubwa Ruth K.

•Kuna uwezekano mkubwa Sonnie alikuwa akimdhihaki mchekeshaji huyo kwa kukana kuwa baba wa bintiye.

Carrol Sonnie, Ruth K, Mulamwah
Image: INSTAGRAM

Muigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie alitoa jibu la kejeli kwa habari za aliyekuwa mpenzi wake, mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah kudokeza anatarajia mtoto na rafiki yake mkubwa Ruth K.

Mnamo Jumanne, Mulamwah na Ruth K ambao wamedaiwa kuwa katika uhusiano wa kimapenzi licha ya kukanusha waziwazi walidokeza kuwa wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja.

Wasanii hao wawili ambao wamekuwa wakidai kuwa ‘besties’ tu walishiriki machapisho sawa yaliyopendekeza kuwa Ruth ana dalili za ujauzito.

“Natapika tapika asubuhi asubuhi hivi na kuchoka choka, inaweza kua nini,” Ruth aliposti kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Kwa upande wake, Mulamwah aliandika, “Bestie anatapika tapika ma asubuhi asubui ivi. Shida inaweza kua nini?"

Ingawa hawakuthibitisha ikiwa kweli walikuwa wakizungumza kuhusu ujauzito, wengi waliamini kwamba wawili hao walikuwa wakidokeza kutarajia mtoto pamoja.

Blogu moja ya humu nchini iliripoti kuwa wasanii hao wawili walionekana kuthibitisha kuwa ni kweli Ruth ni mjamzito kama ambavyo imekuwa ikidaiwa siku za hivi majuzi.

Wakati akijibu chapisho hilo kwenye mtandao wa Instagram, Carrol Sonnie alitoa maoni ya dhihaka akisema, "Keila sio mtoto wangu wamepata mtoto."

Kuna uwezekano mkubwa Sonnie alikuwa akimdhihaki mchekeshaji huyo kwa kukana kuwa baba wa bintiye na baadaye kudaiwa kumpa ujauzito mwanamke mwingine.

Image: INSTAGRAM// NAIROBI GOSSIP

Mapema mwezi jana, Mulamwah alisema hana uhakika kama 'bestie' wake Ruth K ni mjamzito kama ambavyo Wakenya wamekuwa wakikisia.

Katika mahojiano na wanahabari, mchekeshaji huyo alifichua bado hakuwa amepata dokezo lolote kwamba Ruth anatarajia mtoto wake wa kwanza.

“Mimi sijui, mimi sijui, mimi siwezi kutarajia mtoto, ningekuwa nimesikia akigonga kwa tumbo. Lakini nitamuuliza,” Mulamwah alisema.

Mchekeshaji huyo alishikilia kuwa mrembo huyo ambaye amekuwa akiigiza naye ni rafiki yake tu na hakuna uhusiano wa kimapenzi kati yao.

Kuhusu tetesi za kumtunga ujauzito mwigizaji huyo, alisema kuwa huenda mlimbwende huyo  na mpenzi wake wameamua kupata mtoto.

“Sijajua. Mimi nitamuuliza. Labda wameamua na mpenzi wake, sijui,” alisema.

Aliongeza, “Mimi huwaambia ako na chali yake kwa hivyo maisha yake siwezi kuingilia, labda mimi niulize kama nyinyi, jambo ambalo sio sahihi kwangu kufanya. Kama ni kitu atataka tujue basi bila shaka atatuambia.

Kwa upande wake, Mulamwah aliweka wazi kuwa bado yuko sokoni kwani kwa sasa hana uhusiano wa kimapenzi na mtu yeyote.