Baada ya kuzua tafrani na 'Nataka Kunyonywa', Embarambamba awakosha mashabiki na 'Panua'

Sehemu ya wimbo huo iliimba akimtaka Mungu kupanua kwa njia ambayo iliwaacha wengi katika njia panda wakidhani huenda anaimba mambo tofauti na injili.

Muhtasari

• Unaeleza wimbo huo: “Panua Yesu, panua wagonjwa wapone…panua maisha yetu…”

• Hata hivyo, majina anayozipa nyimbo zake yamezua gumzo miongoni mwa Wakenya, baadhi wakisema anawapotosha mashabiki wake.

Embarambamba
Embarambamba
Image: Screengrab

Msanii wa injili mwenye utata kutoka kaunti ya Kisii, Embarambamba amerejea tena na kibao kingine chenye utata kama kawaida yake.

Baada ya kuzua minong’ono mitandaoni wiki chache zilizopita na kibao chake cha ‘Nataka Kunyonywa’ msanii huyo tena amegonga pale pale kwenye mshono na kibao kingine chenye utata kwa jina ‘Panua’.

Mwanamuziki huyo, alitoa kibao hicho mnamo Jumapili, mistari yake ikizua migawanyiko mikubwa miongoni mwa mashabiki wake.

Sehemu ya wimbo huo iliimba akimtaka Mungu kupanua kwa njia ambayo iliwaacha wengi katika njia panda wakidhani huenda anaimba mambo tofauti na injili.

Unaeleza wimbo huo: “Panua Yesu, panua wagonjwa wapone…panua maisha yetu…”

Kabla ya nyimbo hizo mbili, alikuwa pia ametoa kibao ‘Nimwagie’, ambacho pia alidai ni cha injili, na lengo lake kuu ni kumtukuza Mungu.

Hata hivyo, majina anayozipa nyimbo zake yamezua gumzo miongoni mwa Wakenya, baadhi wakisema anawapotosha mashabiki wake.

Licha ya wengi kuhisi kwamba anaimba mambo ya kutukuza anasa akijificha ndani ya joho la utakatifu, Embarambamba katika mahojiano na chaneli ya 2Mbili alikana akisema kwamba yeye anaimba injili ila Wakenya wengi ndio wanaomchukulia vibaya wakiwa na fikira za anasa.

“Mimi huwa namuimbia Mungu Lakini sasa wananchi, eehee… walikuwa wanahariri na kukata pale penye nimeimba ‘ninyonye’ wanaweka mitandaoni mpaka hata wewe ukiangalia unajiuliza hii ni injili kweli?” Embarambamba alisema.

Hata hivyo, msanii huyo amekuwa akitetea hatua ya kutumia maneno kama hayo ambayo yanachukuliwa na kizazi cha sasa nje ya muktadha.