Akothee atoa onyo kali kwa wanaomhusisha na Schweizer, atishia kuchukua hatua za kisheria

Akothee alionya kwamba wale hawatatii onyo lake wanaweza kujikuta mahakamani wakishtakiwa kwa kuchafuliana jina.

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alitishia kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote anayemhusisha na mwanaume huyo kutoka Uswizi.

•Wakati wa kipindi hicho  alimuita meneja wake Nelly Oaks "babe" na kubainisha kwamba hana jina lingine la kumwita.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee ametoa onyo kali kwa wanaomhusisha na mumewe mzungu Denis ‘Omosh’ Schweizer.

Wakati akiwahutubia wafuasi wake kwenye kipindi cha moja kwa moja kwenye Facebook siku ya Jumatano, mama huyo wa watoto watano alitishia kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote anayemhusisha na mwanaume huyo kutoka Uswizi.

Akothee alionya kwamba wale ambao hawatatii onyo lake wanaweza kujikuta mahakamani wakishtakiwa kwa kuchafuliana jina.

"Iwapo utathubutu kuniita Schweizer, nitakupeleka mahakamani kwa kuchafuliana jina," Akothee alisema kwenye Facebook.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 hata hivyo hakufichua kwa nini hasa hataki kuhusishwa na mwanamume huyo aliyefunga ndoa naye mnamo Aprili 10.

Wakati wa kipindi hicho cha moja kwa moja, alimuita meneja wake na mpenzi wake wa zamani, Nelly Oaks "babe" na kubainisha kwamba hana jina lingine la kumwita. Pia alidokeza kuwa Nelly daima atakuwa sehemu ya maisha yake

“Sina jina lingine la kumuita. Jinsi unavyochagua kutafsiri sio wasiwasi wangu. Kuna sifa fulani ninazozipenda kwa mtu huyu, na nimewasiliana naye. Nilimwambia, ‘Jua tu kwamba hata ikiwa hatutawahi kuoana, mjulishe mke wako kwamba kuna mwanamke anayeitwa Akothee ambaye atakuwa sehemu ya maisha yako daima’,” alisema.

Katika siku za hivi majuzi, Akothee amekuwa akionekana sana akiwa pamoja na meneja wake Nelly Oaks na kuwafanya wanamtandao kutilia shaka uhusiano wao halisi.

Hivi majuzi, mwanamuziki huyo hata alifichua kuwa Nelly bado amehifadhi namba yake kama ‘Babe’ kwenye simu yake licha ya uhusiano wao kuisha mwaka jana.

“Huyu jamaa (Nelly Oaks) hajawahi badilisha jina langu kutoka Babe na kuwa Esther au AKOTHEE 🤔🤔🤔🤔🤔🤔. Hii ilikuwa 2021. Nitampa @nellyoaks zawadi ambayo itawashtua wengi 🤣🤣🤣🤣🤣” Akothee aliandika siku ya Jumatano chini ya picha yake na Nelly Oaks iliyopigwa mwaka wa 2021.

Huku mwanamuziki huyo akionekana kuendelea kuwa karibu zaidi na mpenzi wake wa zamani Nelly Oaks, pengo kubwa linaonekana kuongezeka kati yake na mumewe Bw Schweizer lakini bado hajafichua ikiwa ndoa yao bado iko sawa.