Karen Nyamu afunguka jinsi bintiye anavyo'wacheza' babake mzazi, DJ Saint Kevin na Samidoh

Karen Nyamu alifichua kuwa tayari amewatambulisha watoto wa Samidoh na Edday Nderitu kwa binti yake.

Muhtasari

•Karen alifichua kuwa msichana huyo mwenye umri wa miaka tisa anawatambua Samidoh na DJ Saint Kevin kama baba zake.

•Alifichua kuwa huwa anajaribu kumueleza msichana huyo wa miaka tisa kuhusu hali nzima katika familia yake.

(Kulia) Karen Nyamu, mpenzi wake Samidoh na familia yao, (Kushoto) DJ Saint Kevin
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amefunguka kuhusu suala la malezi ya watoto wake na kufichua uhusiano mzuri kati ya bintiye mkubwa Tiana na baba zake wawili.

Katika mahojiano kwenye chaneli ya YouTube ya Convo, mama huyo wa watoto watatu alifichua kuwa msichana huyo mwenye umri wa miaka tisa anawatambua Samidoh (mpenzi wa sasa wa Karen Nyamu) na DJ Saint Kevin (mzazi mwenzake Karen Nyamu) kama baba zake.

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi alisema Teana huwaita wanaume wote wawili hao ‘baba’ na hata kufanya nao mazungumzo mara kwa mara.

"Huwa anawaita baba wote wawili 'dad'. Na huwa ninamwambia "una bahati sana kuwa na baba wawili," Karen Nyamu alisema.

Aliongeza, “Huwa anapiga simu kwa mmoja anamwambia “Nataka hiki, hiki na hiki” alafu anapigia huyu mwingine anamwambia, “Nataka hiki na hiki."

Wakili huyo pia alifunguka kuhusu uhusiano wake na binti yake akifichua kuwa kwa kawaida huwa anashiriki mazungumzo naye kuhusu masuala mbalimbali ya kifamilia.

Alifichua kuwa huwa anajaribu kumweleza msichana huyo wa miaka tisa kuhusu hali nzima katika familia yake ili asishangae wakati akisoma mambo kwenye mitandao ya kijamii.

“Mtoto wangu ako na simu, ako na tablet. Shule pia wako na stori za internet. Kawaida mimi huwa na mazungumzo na mzaliwa wangu wa kwanza, amefikisha umri wa miaka tisa hivi majuzi. Kawaida huwa nashiriki mazungumzo naye kwa sababu kuna vitu atakutana nazo mitandaoni,” alisema.

Karen Nyamu aliendelea kufichua kuwa tayari amewatambulisha watoto wengine wa Samidoh na mke wake wa kwanza, Edday Nderitu kwa bintiye.

“Kama familia hiyo nyingine, anawajua wote kwa majina. Kutoka kwa mama, watoto. Anawajua, mimi nimemwambia. Nimejaribu kumueleza vile hali iko. Hatapata mshangao mtandaoni. Anahitaji kukabiliana nayo pia tusikuwe na siri mimi na yeye, eti anaweza ona kitu imchanganye ama apate masuala ya kisaikolojia. Ninazungumza naye kwa upole, huwa namwambia haya mambo,” seneta Nyamu alisema.

Seneta huyo wa kuteuliwa wa UDA alifichua kwamba hata huwa anamwonyesha binti huyo wake wa miaka tisa baadhi ya maneno makali yaliyoelekezwa kwake kwenye mitandao ya kijamii ili kumfahamisha na mambo kama hayo.

Karen Nyamu ana watoto wawili na mpenzi wake wa sasa Samidoh, Samuel Muchoki Jr na Taraya Wairimu. Binti yake wa kwanza, Teana ni mtoto wake na mpenzi wake wa zamani DJ Saint Kevin.