Nanny Rozzie afunguka kuhusu uhusiano na Cartoon Comedian

Wakenya wengi wamekuwa wakimfananisha Rozzie na mchekeshaji Cartoon Comedian.

Muhtasari

•Roseline Atieno amekanusha kuwa na uhusiano na mchekeshaji Vanessa Akinyi almaarufu Cartoon Comedian.

•Rozzie aliweka wazi kuwa hana uhusiano wa damu na mchekeshaji huyo na hata akabainisha kuwa hamfahamu.

Nanny Rozzie na Cartoon Comedian
Image: HISANI

Mwanadada wa Kenya ambaye amekuwa akivuma sana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Roseline Atieno almaarufu ‘Rozzie’ amekanusha kuwa na uhusiano na mchekeshaji Vanessa Akinyi almaarufu Cartoon Comedian.

Tangu kupata umaarufu siku chache zilizopita baada ya kusambaa kwa video yake yenye hisia kali akiaga familia ya mwajiri wake kutoka Lebanon, wanamitandao wengi wamebaini kufanana kwa kiasi kikubwa kati ya mama huyo wa watoto wawili anayetoka Kaunti ya Siaya na Cartoon Comedian.

Katika mahojiano na Bennie Experience hata hivyo, Rozzie aliweka wazi kuwa hana uhusiano wa damu na mchekeshaji huyo na hata akabainisha kuwa hamfahamu.

“Hapana, simfahamu. Hatuna uhusiano,” alisema.

Wakenya wengi wamekuwa wakimfananisha Rozzie na Cartoon Comedian huku kundi hata likidai kuwa kuna uwezekano mkubwa wao ni dada.

Rozzie ambaye amekuwa akifanya kazi nchini Lebanon kwa miaka miwili iliyopita hata hivyo anatoka Siaya ilhali Cartoon Comedian alizaliwa na kukulia jijini Nairobi.

Katika siku kadhaa zilizopita, video inayoonyesha nyakati za kihisia wakati Rozzie, wanandoa aliokuwa akiwafanyia kazi na watoto wao wanne wakiagana imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakionekana kuguswa sana na upendo ulioonyeshwa.

Katika mahojiano hayo, mama huyo wa watoto wawili alieleza sababu kuu kwa nini watoto wa mwajiri wake waliwezwa na hisia wakati alikuwa akiondoka Lebanon.

"Nadhani ni upendo wa mama tu ambao nimekuwa nikiwapa kwa sababu pia nina watoto. Nilikuwa nikiwachukulia kama watoto wangu tu,” Rozzie alisema.

Wakati uo huo, mwanadada huyo kutoka Kaunti ya Siaya alikanusha madai kwamba watoto aliokuwa akiwatunza walikuwa karibu sana naye kwani mwajiri wake alikuwa amewatelekeza.

"Sio kweli, alikuwa kila wakati kwa watoto wake," alisema.

Rozzie alisema kwamba alifahamu kuhusu video yake inayovuma kutoka kwa rafiki yake anayeishi Lebanon baada ya kuwa tayari imeanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

"Nilifurahia .. familia ya Lebanon ilikuwa na furaha kwangu," alisema.

Akizungumzia kazi yake nchini Lebanon, alifichua kwamba aliondoka Kenya kuelekea hiyo  ya Mashariki ya Kati mnamo 2021 ili kutafuta pesa za kumsaidia kuwatunza watoto wake wawili.

Alifichua kuwa amerejea Kenya kwa likizo kisha anapanga kurejea Lebanon.

"Nitarudi.. nikipewa kazi nchini Kenya nitafanya kazi," alisema.