Kate Actress azungumzia kurudiana na aliyekuwa mumewe, Phil Karanja

Waigizaji hao wawili mashuhuri walitangaza kuachana kwao Septemba baada ya miaka kadhaa ya ndoa.

Muhtasari

•Wawili hao walikuwa wameandaa karamu ya siku ya kuzaliwa ya binti yao ambaye alitimiza miaka minne mnamo Desemba 15.

•Wakati aliposhinikizwa kurudiana na baba huyo ya bintiye, Kate aliweka wazi kwamba hakuna uwezekano wa hilo kutokea.

Phil Karanja, Kate Actress na binti yao Njeri wakati wa karamu ya siku ya kuzaliwa
Image: FACEBOOK// KATE ACTRESS

Muigizaji mashuhuri wa Kenya Catherine Kamau almaarufu Kate Actress hivi majuzi alijibizana vikali na baadhi ya mashabiki wake kwenye mtandao wa Facebook baada ya kuchapisha picha zake na aliyekuwa mume wake, Philip Karanja almaarufu Phil Director.

Waigizaji hao wawili ambao walitangaza mwisho wa ndoa yao takriban miezi mitatu iliyopita walikuwa wameandaa karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya binti yao ambaye alitimiza miaka minne mnamo Desemba 15 na Kate Actress baadaye alishiriki picha zilizopigwa kwenye hafla hiyo nzuri.

Katika sehemu ya maelezo ya chapisho lake, mama huyo wa watoto wawili alizungumza kuhusu uhusiano mzuri kati ya bintiye na mzazi mwenzake Phil Karanja.

"Yeye ndiye mtu mdogo anayependwa zaidi ulimwenguni. Msichana wa baba katika kila kitu. Alikuwa na siku nzuri ya kuzaliwa, "Kate Actress alisema kwenye picha alizochapisha

Idadi nzuri ya watumiaji wa Facebook waliopata kuona chapisho hilo walionekana kuangazia zaidi picha zilizomuonyesha Phil Karanja. Wengine hata walichukua hatua zaidi kuelezea jinsi waigizaji hao wawili walivyoonekana vizuri pamoja na kuwataka warudiane.

Zainb Nyamweno alisema, “Aki shetani hutoka wapi hakika? Jinsi mnavyoonekana vizuri pamoja, heri ya kuzaliwa kasupuu."

"Aki tunawekeleanga shetani saa zingine.. uhusiano ni chaguo la kibinafsi," Kate Actress alijibu/

Mwanamtandao mwingine, Zippy Kibe alisema, "Tunaomba muungano tena.."

Kate akajibu, “Ya Ruto na baba?

Wakati aliposhinikizwa kurudiana na baba huyo ya bintiye, muigizaji huyo wa zamani wa kipindi cha ‘Mother in Law’ aliweka wazi kwamba hakuna uwezekano wa hilo kutokea.

"Napenda hili... na mrudiane mnaonekana vizuri pamoja," Essie Paul aliandika.

Kate alijibu kwa ujasiri, "Hatuwezi!"

Huku akimjibu shabiki mwingine aliyemshinikiza arudiane na Phil, mama huyo wa watoto wawili pia alibainisha wazi kuwa yeye huwa hana tamaa ya kuwa na mwanaume fiulani kwani yeye ndiye huamua kuchagua anayetaka kuwa naye maishani.

"Mimi sio aina ya kukata tamaa! Ninapata kuchagua ninayemtaka, ninapotaka, sio vinginevyo. Mimi ni daraja la juu. Wewe ni pickmeisha. Kwaheri,” alisema.

Kate na Phil walitangaza talaka yao katikati ya Septemba baada ya kufurahia ndoa kwa miaka kadhaa.

Walikuwa wamebadilishana viapo vyao mnamo Novemba 2017 katika hafla ya kipekee iliyohudhuriwa na marafiki wa karibu na familia pekee.