Justina Syokau aahidi kutoimba wimbo wa 2024 baada ya Wakenya kumsihi asiwarogee mwaka

“Nataka kuwaambia Wakenya, sitauchokoza mwaka. Sio tu uchokozi, mimi sitawarogea mwaka," Justina alisema.

Muhtasari

•Mwimbaji Justina Syokau ameahidi kutoimba wimbo maalum wa mwaka wa 2024 tunapojiandaa kuuaga mwaka wa 2023.

•Justina alifichua watu wamekuwa hawampi amani anapopita mjini kwani wamekuwa wakimsimamisha na kumwagiza asiimbe wimbo wa 2024.

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Justina Syokau
Mwanamuziki wa nyimbo za injili Justina Syokau
Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za Injili mwenye utata Justina Syokau almaarufu Madam 2020 ameahidi kutoimba wimbo maalum wa mwaka wa 2024 tunapojiandaa kuuaga mwaka wa 2023.

Katika video ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii, mwanamuziki huyo ambaye anafahamika sana kwa wimbo wake '2020' alioutoa miaka michache iliyopita katika kusherehekea mwaka 202,  alisema kuwa mashabiki wengi wameibua malalamiko dhidi yake na kumsihi asitoe wimbo wa mwaka 2024.

Justina alibainisha kuwa licha ya kwamba watu wengi aliokutana nao wamekuwa wakimuomba asichokoze mwaka ujao kwa kuuimbia, hana nafasi katika masaibu yoyote ambayo yamewapata watu katika miaka ya nyuma.

“Watu wanasema 2024 usiimbe, wanasema nisichokoze mwaka. Watu wanasema niache 2024 ije bila kuchokozwa, nisiimbie 2024,” Justina Syokau alisema kwenye video hiyo.

Aliongeza, “Nataka kuwaambia Wakenya kwamba mimi kama Justina Syokau, sitauchokoza mwaka. Sio tu uchokozi,  mimi sitawarogea mwaka, na sirogangi. Watu wananiwekea mashida zao, nataka kuwaambia mimi siimbi wimbo wa 2024 na tafadhali nataka muwe na amani.”

Mama huyo wa mtoto mmoja alifichua kuwa watu wamekuwa hawampi amani anapopita mjini kwani wamekuwa wakimsimamisha na kumwagiza asiimbe wimbo wa mwaka ujao.

“Jameni sio mimi nimekuleteea mashida ambazo uko nazo, sishiriki. Sina ushiriki sifuri katika maeneo ambayo umeshindwa mwaka huu. Kama hukupanuliwa mipaka, ni wewe. Kama mwaka wako haukuzaa matunda, ni wewe,” alisema huku akibainisha kuwa kwa upande wake amebarikiwa sana katika mwaka unaoelekea ukingoni.

Alisema kuwa mwaka wa 2023 alikutana na mpenzi wa maisha yake na akabainisha kuwa anafurahia ndoa yake.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili pia alitumia fursa hiyo kuwashauri wanawake kuwadekeza vyema waume zao ili kuimarisha ndoa zao.