Mama Dangote afichua kwa nini Diamond bado hajaoa, asema mwanawe na Zuchu "wanachezeana"

Alieleza kuwa mahusiano ya Diamond na Zuchu ni ya kuchezeana kwani hakuna taratibu za ndoa zilizofanyika.

Muhtasari

•Bi Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote amesema kuwa Mungu bado hajamuelekeza bosi huyo wa WCB kufunga ndoa.

•“Kama mtu hajatoa barua, ni kutembea tu. Hiyo inaitwa kuchezeana. Huyo (Zuchu) sio mchumba, huyo ni mwanamke tu,” Mama Dangote alisema

Mama Dangote amejibu kuhusu kuzozana na Zuchu
Image: HISANI

Mama mzazi wa mwimbaji wa Bongo, Diamond Platnumz, Bi Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote amesema kuwa Mungu bado hajamuelekeza bosi huyo wa WCB kufunga ndoa.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Wasafi Media, alibainisha kuwa ndoa hufanyika tu kulingana na mipango ya Mwenyezi Mungu.

“Kila kitu Mungu ndiye huwa amepanga. Yeye (Diamond) anaweza kujisukuma, na mimi naweza kumskumiza lakini kila kitu kinatokana na Mungu anavyokuamrisha. Mungu anaweza kuamrisha umuoe fulani, au Mungu anaweza kukuamrisha umuoe huyu mwingine,” Mama Dangote alisema.

Alisema hawezi kumshinikiza Diamond kufunga ndoa na mtu yeyote kwa sababu huenda mtu huyo akawa si yule ambaye Mungu alitaka awe naye.

“Anaweza kukaa na hata wanawake mia lakini Mungu awe hajamuamrisha kuwaoa. Maanake huenda Mungu ameamrisha huyo atamuoa mtu fulani,” alisema.

Mama Diamond alibainisha kuwa katika siku za nyuma kabla ya kuolewa na Uncle Shamte, pia amakuwa na wanaume wengi ambao hawakumuoa licha ya hata kuzaa.

"Yote ni mipango ya Mungu," alisema.

Mama Dangote pia alifichua kuwa mwanawe bado hajamtambulisha mtu yeyote kama mke wake licha ya tetesi nyingi kuwa mwimbaji huyo anatoka kimapenzi na malkia wa bongo fleva Zuhura Othman almaarufu Zuchu.

Alieleza kuwa mahusiano yanayodaiwa ya Diamond na msanii huyo wa kike wa WCB ni ya kuchezeana kwani hakuna taratibu za ndoa zilizofanyika.

“Kama mtu hajatoa barua, ni kutembea tu. Hiyo inaitwa kuchezeana. Huyo (Zuchu) sio mchumba, huyo ni mwanamke tu,” Mama Dangote alisema.

Aliongeza, “(Diamond) hajawahi kuniletea Zuchu eti anataka kumuoa. Mimi kwanza najua Zuchu ni msanii wake. Kusema eti Zuchu ni mchumba wake sijui, kwa sababu mimi sijapeleka mahari kwa kina Zuchu wala barua. Zuchu namjua ni msanii wake. Kila siku tuko naye sijui. , najua ni msanii. Mimi ninachojua mchumba ni yule ambaye unapeleka barua na mahari."

Hata hivyo alisusia kujibu iwapo anaunga mkono uhusiano wa mastaa hao wawili wa bongo fleva akibainisha kuwa wao wenyewe ndio wataamua.

Pia alibainisha kuwa Zuchu si mwanamke wa kwanza kuhusishwa kimapenzi na mwanawe kwani amekuwa akidaiwa kutoka na wanawake wengine wengi waliowahi kuonekana naye katika siku za nyuma.