Edday akirudi kwa mix hawezi kuwa tatizo- Karen Nyamu azungumzia ziara ya Samidoh Marekani

Seneta huyo wa kuteuliwa alifichua kuwa Samidoh alienda Marekani ili tu kuwaona watoto wake.

Muhtasari

•Alibainisha wazi kwamba hakutakuwa na tatizo kama Samidoh ataamua kusuluhisha mambo na mke wake wa kwanza, Bi Edday Nderitu.

•Aliweka wazi kuwa hatajiunga na Samidoh na familia yake nyingine Marekani kwani ingeharibu mambo, kinyume na matakwa yao.

Karen Nyamu na mpenzi wake Samidoh
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Binti mkubwa wa Samidoh, Shirleen Muchoki mnamo Jumatatu asubuhi alithibitisha kwamba mwimbaji huyo maarufu wa Mugithi yuko pamoja nao nchini Marekani.

 Shirleen alithibitisha ufichuzi wa awali wa seneta Karen Nyamu ambaye alitangaza habari kuhusu ziara ya Samidoh mwishoni mwa wiki jana katika moja ya posti zake.

Wakati akimjibu shabiki wake mmoja katika moja ya machapisho yake ya hivi majuzi kwenye mtandao wa Facebook, seneta huyo wa kuteuliwa alifichua kuwa Samidoh alienda Marekani kuwaona watoto wake. Pia alitumia fursa hiyo kubainisha wazi kwamba hakutakuwa na tatizo lolote kama mwimbaji huyo wa Mugithi ataamua kusuluhisha mambo na mke wake wa kwanza, Bi Edday Nderitu..

"Yeye (Samidoh) yuko pale tunapozungumza kuwaona watoto. Eddy pia akirudi kwa mix tumeshare miaka mingi sana kwa amani hatawahi kuwa tatizo,” Karen Nyamu alisema Ijumaa.

Zaidi ya hayo, aliweka wazi kuwa hatajiunga na Samidoh na familia yake nyingine nchini Marekani kwa kuwa ingeharibu mambo, kinyume na matakwa yao.

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Jumatatu asubuhi, ilibainika kwamba Samidoh kwa sasa yuko jijini Boston, Marekani ambapo amepata fursa ya kukutana na watoto wake baada ya muda mrefu.

Bado haijabainika wazi ni lini mwanamuziki huyo mahiri wa Kikuyu alitua katika nchi hiyo ya Magharibi lakini bintiye Shirleen Muchoki alifichua habari za mkutano wao.

Malkia huyo mdogo alitumia ukurasa wake wa Instagram kuelezea furaha yao kwa kukutana na mzazi huyo wao na kufunguka jinsi walivyompeza.

"Wow, siku nzuri sana, baba yangu hatimaye yuko hapa, tumeku’miss baba, karibu Boston," Shirleen alisema katika chapisho lake la Jumatatu asubuhi.

Alionyesha picha nzuri za mwimbaji huyo Mugithi akishiriki wakati mzuri pamoja naye na kaka yake mdogo kwenye uwanja wa ndege. Bi Edday Nderitu na mtoto wao mdogo zaidi hata hivyo hawakuonekana popote kwenye picha, haijabainika iwapo walikuwa pale.

Huenda hii ndiyo mara ya kwanza kwa Samidoh kukutana na watoto wake baada ya miezi mingi sana.